Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaaga viongozi wa dini 104 ambao wanaelekea Dodoma kwa treni ya mwendokasi (SGR) kwenda kushiriki ibada maalum ya kuliombea Taifa inayotarajiwa kufanyika kesho, Jumatatu, Aprili 22, 2024.
Treni hiyo imeondoka stesheni ya Dar es Salaam saa 8.53 mchana ikiwa na viongozi hao, waandishi wa habari, waimbaji wa nyimbo za injili na kaswida, viongozi wastaafu wa Serikali, watendaji wa Shirika la Reli nchini, wawakilishi wa ubalozi na watedaji wengine wa Serikali.
Amewaaga viongozi hao na watendaji wengine wa Serikali na taasisi mbalimbali leo (Jumapili, Aprili 21, 2024) kwenye hafla fupi iliyofanyika kwenye stesheni ya Tanzanite, barabara ya Sokoine, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na viongozi hao kabla ya kupata dua ya kuombea safari yao, Waziri Mkuu amesema: “Leo ni siku muhimu na ya kihistoria kwa nchi yetu. Tuko kwenye wiki ya maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano na tunashuhudia safari ya kwanza ya treni ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma.”
Amesema Tanzania inathamini dini na kutoa uhuru wa wananchi wake kokote na ndiyo maana amani, utulivu na mshikamano vinakuwepo nchini. “Tanzania ni nchi iliyoteuliwa na Mungu kwa utulivu wake, amani na uvumilivu.”
“Hali hii haijaja bure, bali imetokana na juhudi zenu viongozi wa dini. Mahubiri yenu yamesaidia kuwafanya waamini kile ambacho Mwenyezi Mungu ametujalia. Na leo Tanzania imekuwa kimbilio kwa nchi zote zilizokosa amani,” amesema.
Amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kuleta maendeleo na hasa kuboresha miundombinu kwenye maeneo mengi ikiwemo reli, maji, usafiri wa anga, na barabara.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, amesema majaribio yanayofanyika sasa yanahusisha vichwa vya treni, mabehewa na mifumo ya umeme. “Hii ni mara ya kwanza tunaenda Dodoma, lakini tumejipanga ili ifikapo Julai, mwaka huu usafiri wa treni ya abiria kutokea Dar hadi Dodoma uwe umeanza kama Mheshimiwa Rais Samia alikuwa ameagiza.”
Mapema, akitoa taarifa ya mradi huo mbele ya Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa, alisema mradi wote utagharimu dola za Marekani bilioni 10.016 sawa na sh. trilioni 23.33 kwa ajili ya ujenzi wa kilometa 1,596. “Kati ya hizo, kilomea 1,219 ni za njia kuu na kilometa 377 ni za njia za kupishana,” alisema.
Alisema ujenzi huo unahusisha vipande vitano, ambapo kipande cha kwanza (Dar-Moro) kimefikia asilimia 98.93; kipande cha pili cha Morogoro – Dodoma (asilimia 96.61); cha tatu cha Makutupora ya Singida – Tabora (asilimia 24.2); cha nne cha kutoka Tabora hadi Isaka (asilimia 6) na cha tano cha kutoka Isaka – Mwanza (asilimia 56).
Kuhusu vifaa ambavyo vimekwishawasili, Kadogosa amesema: “Tulianza majaribio tangu Februari, 2024 baada ya kupokea vichwa vya treni. Hadi kufikia Aprili 2024, mabehewa 65 yamepokelewa, seti moja ya kichwa cha kisasa (mchongoko) na vichwa tisa kati ya 17 vimeshawasili. Bado tunasubiri mabehewa ya mizigo.”