Tarehe 3 Mei kila mwaka waandishi wa habari duniani huadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari (World Press Freedom Day-WPFD).

Ni siku adhimu si tu kwa waandishi wa habari bali kwa wadau wa sekta ya habari. Ni siku ambayo wadau wa sekta hii hutafakari kwa kina majukumu ya vyombo vya habari, hali ya uhuru wa habari, usalama wa waandishi wa habari, utendaji wa vyombo vya habari na mabadiliko mbalimbali yanayojitokeza kwenye sekta hii muhimu duniani.

Wakati tukiadhimisha siku hii na kwa kuzingatia muktadha wa nchi yetu, napenda kuwatafakarisha masuala machache kama ifuatavyo:

  1. Kauli mbiu ya mwaka huu: Maadhimisho ya mwaka huu yanabebwa na kauli mbiu hii “A Press for the Planet: Journalism in the Face of the Environmental Crisis.” Kauli mbiu hii inaonesha umuhimu wa kuwa na vyombo vya habari huru ambavyo vinahabarisha wananchi, vinasimamia viongozi na kuchochea hatua chanya kuhusu changamoto mbalimbali za mazingira na hatimaye kuifanya dunia iwe sehemu salama ya kuishi.

Mazingira ni kila kitu ikiwemo rasilimali za asili ambazo nchi yetu imejaaliwa kuwa nazo. Ni wajibu wa vyombo vya habari kuhakikisha vinalinda na kusimamia rasilimali hizi ili zitumike kwa maslahi mapana ya nchi na jamii kwa ujumla. Waandishi wa habari kama kizazi cha sasa wanaowajibu wa kuhakikisha rasilimali tulizonazo si tu zinatumiwa vizuri kukidhi maslahi ya kizazi cha sasa, bali zinalindwa na kutunzwa kwa wivu mkubwa kuhakikisha manufaa yake yanavifikia vizazi vijavyo.

Profesa Paul Collier kwenye kitabu chake “The plundered planet: why we must–and how we can–manage nature for global prosperity”, anaandika “We are custodians of the value of natural assets. We are ethically obliged to pass on to future generations the equivalent value of the natural assets that we were bequeathed by the past.”

Kwa ufupi, anachosema Profesa Collier ni hiki: Kama tumeikuta mbunga ya Serengeti yenye wanyama wengi wa kuvutia au ardhi yenye madini mengi, hii ni kwa sababu, babu, bibi na baba zetu (kizazi kilichotutangulia) walitunza rasilimali hizi na kutuachia sisi.

Hivyo basi, na sisi kizazi cha sasa tunawajibu wa kuhakikisha tunatunza thamani ya rasilimali hizo kwa kuzitumia kwa uangalifu ili watoto, wajukuu na vitukuu vyetu vije kufaidi—na si kuacha mbunga isiyokuwa na wanyama au ardhi yenye mashimo. Kwa kuwa leo tunaadhimisha siku hii muhimu, ni wajibu kujiuliza swali hili na kujipima ni kwa kiwango gani vyombo vya habari na waandishi nchini wamesimamia suala hili.    

  • Dhima ya vyombo vya habari: Vyombo vya habari vina majukumu mbalimbali, lakini majukumu mama ni matatu. Vinawajibika kutoa taarifa sahihi na zenye manufaa chanya kwa wananchi, kutengeneza majukwaa ya mijadala ambayo yataibua masuala mbalimbali na kuyajadili kwa faida ya jamii nzima na kusimamia uwajibikaji wa umma. Profesa Franz Kruger aliwahi kusema vyombo vya habari vinapoacha kuibua mijadala vinabaki kuwa wapiga kelele. Wakati tunaadhimisha siku hii, hatuna budi kujiuliza maswali haya: Je, ni kwa kiasi gani vyombo vya habari nchini vinatoa habari zenye manufaa chanya kwa wananchi? Je, habari hizo zinatoa uwiano linganifu kwa makundi yote kwenye jamii? Je, vinatengeneza majukwaa yenye kuibua mijadala yenye afya kwa jamii? Je, vinaibua mijadala yenye kusimamia uwajibikaji?  
  • Umahiri wa taaluma ya habari. Maudhui ndio bidhaa kuu inayozalishwa na kuuzwa na vyombo vya habari. Kwa miaka mitano (5) sasa, tafiti za ubora wa maudhui ya vyombo vya habari zinazotolewa na Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (2017, 2018, 2019, 2020 na 2022) zinaonesha ubora wa maudhui yanayozalishwa na vyombo vya habari nchini umekuwa ukishuka. Wakati tukiadhimisha siku hii muhimu tutafakari kwa pamoja na kuweka nia ya kukuza ubora wa maudhui ya vyombo vya habari. Tuweke nia ya kuzalisha habari tunazozitafuta weyewe na si kutegemea kwa kiasi kikubwa ruzuku za habari, maarufu kama habari za matukio. Tuweke nia ya kuwa na vyombo vya habari vyenye kubeba sauti za pande zote mbili, vyombo vya habari vinavyowasemea wanyonge, wananchi wa kawaida. Tuweke nia ya kusimamia maadili ya uandishi wa habari. Kwa ujumla, tuweke nia ya kusimamia weledi kwenye tasnia hii adhimu.
  • Vyombo vya habari na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa: Mwaka huu (2024), nchi yetu itakuwa na uchaguzi wa serikali za mitaa. Tafiti za vyombo vya habari na chaguzi nchini zimebainisha changamoto mbalimbali za uripoti wakati wa uchaguzi: Kutokuwepo kwa uripoti wenye ulinganifu baina ya vyama na wagombea; uripoti wa matukio zaidi kuliko uchambuzi wa mambo ikiwemo sera za vyama; kutoripotiwa kwa kina kwa utekelezaji wa ahadi za wagombea walioko madarakani; kutohojiwa kwa kina kwa ahadi zinazotolewa na vyama na wagombea wakati wa uchaguzi; kutotoa nafasi ya mijadala kwa wananchi na kuacha mchakato mzima wa uchaguzi kutawaliwa na vyama na wagombea; wagombea wanawake kupewa nafasi kidogo ukilinganisha na wagombea wanaume; na kuwepo kwa idadi ndogo wa waandishi wenye uzoefu wa kuripoti uchaguzi. Wakati tunaadhimisha siku hii, tutafakari changamoto hizi na nyingine nyingi kwa lengo la kukuza ubora wa uripoti wa uchaguzi wa serikali za mitaa na baadaye mwakani uchaguzi mkuu.      
  • Vyombo vya habari na maslahi ya taifa: Vyombo vya habari vinawajibika kusimamia maslahi ya taifa. Habari zinazotolewa zinachangia muingiliano wa jamii, kuimarisha umoja, amani na mshikamano. Wakati tukiadhimisha siku hii, vyombo vya habari viendelee kuwa gundi inayoleta umoja wetu, vizalishe maudhui yenye kuchochea mshikamano wetu, viendelee kuipigania mama Tanzania. Viwanyoshee vidole wale wote wanaovuruga amani na mustakabali wa nchi yetu hata kama watu hao ni viongozi. Kwenye hili, vyombo vya habari vifanye kazi ya kuwa wakemeaji wakuu.  

Abdallah Katunzi anafundisha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam — Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma Tanzania. Ana Shahada ya kwanza ya Sayansi ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania, Shahada ya Uzamili ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kutoka Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda. Kwa sasa, anasomea Shahada ya Uzamivu ya Habari na Mawasiliano katika Chuo Kikuu cha Nairobi, Kenya.