Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema Serikali inaendelea na utekelezaji wa
miradi mbalimbali ya umeme itakayoboresha upatikanaji umeme mkoani Songwe ikiwemo
ujenzi wa kituo cha umeme na switching station .

Naibu Waziri  wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga akijibu swali la Mbunge Mbozi, Mhe. George Mwenisongole bungeni jijini Dodoma aliyetaka kufahamu ni lini ujenzi wa Kituo cha upoza Umeme Kakozi, Tunduma utaanza.


Naibu Waziri Kapinga amesema hayo tarehe 8 Mei, 2024 bungeni jijini Dodoma  wakati akijibu
swali la Mbunge Mbozi, Mhe. George Mwenisongole aliyetaka kufahamu ni lini ujenzi wa Kituo
cha upoza Umeme Kakozi, Tunduma utaanza.


Akijibu swali hilo Mhe. Kapinga alisema “Serikali kupitia mradi wa TAZA unaotekelezwa na
TANESCO ipo katika hatua za awali za ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Nkangamo
(Tunduma) kilichopo takribani kilomita 28 kutoka Kijiji cha Kakozi, Mbozi.

Ujenzi wa kituo
hiki  unatarajiwa kuanza hivi karibuni ambapo kwa sasa mkataba kati ya TANESCO na
mkandarasi atakayejenga kituo hiki tayari umeshasainiwa.”


Ameongeza kuwa, kukamilika kwa kituo hicho cha Nkangamo (Tunduma) kutawezesha
upatikanaji wa umeme wa uhakika katika Kijiji cha Kakozi na maeneo mengine ya Jimbo la
Mbozi.
Akizungumzia hali ya upatikanaji umeme kwa ujumla mkoani Songwe, Kapinga amesema kuwa
mkoa huo unapata umeme kutoka kituo cha Mwakibete kilichopo mkoani Mbeya ambapo laini
hiyo ya umeme ni ndefu sana na kupelekea kutokea kwa changamoto za upatikanaji umeme
mkoani Songwe.
Kutokana na hilo amesema Serikali inachukua hatua mbalimbali ikiwemo ya kujengwa
switching station mkoani Songwe pamoja na kituo  cha umeme kitakachojengwa kupitia mradi
wa TAZA huku uboreshaji wa miundombinu ya umeme ukiendelea.


Akijibu swali la Mbunge wa Urambo, Mhe. Margaret Sitta aliyetaka kufahamu ni lini kituo cha
umeme cha Uhuru  kitakamilika, Mhe. Kapinga amesema kituo  kipo ukingoni kukamilika na
hivyo kuboresha hali ya umeme wilayani Urambo.