WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania inaunga mkono uamuzi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) juu ya kuongeza mbinu za uvunaji wa maji, udhibiti wa mafuriko na miundombinu ya kuhifadhi maji hayo ili yatumike wakati wa ukame ama kiangazi kuzuia mafuriko msimu wa mvua nyingi.
“Tanzania inaunga mkono uamuzi huo na inasisitiza Sekretariet ya SADC kuongeza misaada kwa nchi wanachama katika ujenzi wa mabwawa ya kutunza maji ambayo yatatumika katika vipindi vya ukame na kiangazi pamoja na kuzuia mafuriko katika vipindi vya mvua,” amesema.
Waziri Mkuu amesema hayo leo (Jumatatu, Mei 20, 2024) wakati akizungumza kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC kuhusu athari za mvua za El Nino. Ameshiriki mkutano huo kwa njia ya mitandao kutokea ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma.
Maamuzi hayo yaliyopendekezwa kwenye kikao cha Mawaziri wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo yalitaka ziongezwe mbinu za uvunaji wa maji, udhibiti wa mafuriko na miundombinu ya kuhifadhi maji kwa msaada kutoka kwa Sekretarieti ya SADC, Mashirika ya Uendelezaji Mabonde ya Mito (RBOs) na wadau wa maendeleo ili kuongeza nguvu ya kukabiliana na ukame ama mafuriko yanayosababishwa na hali ya hewa kwenye ukanda wa SADC.
Mapendekezo mengine yaliyotolewa ni kuboresha utendaji wa Usimamizi wa Rasilimali za Maji Jumuishi (IWRM); kufuatilia viwango vya maji na kutekeleza huduma za WASH; kuboresha usimamizi wa maji yanayohusisha nchi zaidi ya moja na ushirikiano wa kimataifa; kuhamasisha uhifadhi wa maji na kukuza matumizi ya maji machafu yaliyotibiwa na maji yaliyochujwa chumvi (desalination).
Akielezea kuhusu ujenzi wa mabwawa ya kutunzia maji ambayo yatatumika katika vipindi vya ukame na kiangazi pamoja na kuzuia mafuriko katika vipindi vya mvua, Waziri Mkuu aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo kuwa Serikali ya Tanzania tayari imeandaa Mpango Mkakati wa Ujenzi Malambo 40 Nchini (rain water ponds) kuanzia Novemba 2023 hadi Julai 2024 ambao ni awamu ya kwanza.
“Lakini tuna mkakati kwa ajili ya ujenzi wa malambo (charco dams) katika vijiji vilivyopo maeneo kame ambayo yapo pembezoni mwa barabara kuu ili kuongeza maji yatakayotumika kwa kilimo cha umwagiliaji,” amesema na kuongeza:
“Pia Serikali ina mpango mkakati wa ujenzi na ukarabati wa mabwawa makubwa tuliyonayo kwa lengo la kuwezesha kilimo cha umwagiliaji kwenye maeneo hayo ili kuwa na uzalishaji wa mazao ya chakula kwa kiasi kikubwa.”
Amesema Tanzania itawasiliana na Sekretarieti juu ya mipango ya uvunaji maji ya mvua ambayo imeiandaa.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema Tanzania itaendelea na mipango ya kuhakikisha inaongeza uzalishaji wa chakula ili kuendelea kuwa na ziada ya kutosha kwa mahitaji ya ndani na hata kuuza ziada hiyo nje ya nchi.
Amesema katika kukabiliana na matatizo ya lishe nchini, mkazo mkubwa umewekwa kwenye kuongeza tafiti za uzalishaji wa mbegu zilizoongezewa virutubishi (biofortified) ili kuongeza upatikanaji wa mbegu hizo kwa wakulima na hivyo kuongeza uzalishaji wa mazao na kusaidia katika kuboresha lishe ya jamii hususan kwa watoto chini ya miaka mitano, akinamama wajawazito na wanaonyonyesha.
“Tanzania inaunga mkono mpango wa nchi za SADC kuagiza mazao ya nafaka kutoka nchi wanachama zenye uzalishaji wa ziada wa mazao hayo. Pia tutaendelea kuunga mkono jitahidi za SADC katika kufanya tathmini ya kina ya hali ya usalama wa chakula na lishe. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaunga mkono jitihada zitakazofanywa na sekretarieti ya SADC katika kusaidia nchi wanachama wa SADC zenye upungufu wa nafaka kupata masoko ya nafaka hizo,” amesema.
Akitoa ufafanuzi kuhusu maafa yaliyosababishwa na kunyesha kwa mvua za El Nino na kimbunga HIdaya, Waziri Mkuu aliwaeleza wakuu hao wa nchi kwamba Serikali ilichukua hatua za haraka ili kukabiliana na athari zilizojitokeza. “Hatua hizo ni pamoja na kutoa misaada ya kibinadamu kwa waathirika, kurejesha hali ya majengo na miundombinu ikiwemo barabara, miundombinu ya maji na umeme.”
Washiriki wa mkutano huo walikuwa ni wakuu wa nchi za Angola, Botswana, DRC, Namibia, Lesotho, Zambia, Zimbabwe na Waziri Mkuu wa Eswatini. Washiriki wengine walikuwa ni Mawaziri kutoka Madagascar, Afrika Kusini, Malawi, Msumbiji, Mauritius na Shelisheli.