Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema Serikali inaendelea na utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya Mbalizi-Mkwajuni kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilometa 92 inayounganisha mikoa ya Mbeya na Songwe.
Mhe. Kasekenya ameyasema hayo leo Bungeni jijini Dodoma katika kipindi cha maswali na majibu alipokua akijibu swali la Mbunge wa Viti maalum mkoa wa Songwe Mhe. Stella Fiyao, alietaka kujua Je? mpaka sasa ni kilometa ngapi zimejengwa kwa kiwango cha lami katika barabara ya Mbalizi-Mkwajuni?
“Mhe. Mbunge nikuhakikishie, Mhe.Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari alishatoa maelekezo ya barabara hiyo na sasa tumeshaanza utekelezaji kwa hatua tuko kwenye maandalizi ya kutenga fedha katika bajeti ijayo ili kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo,” amesema Mhe. Kasekenya.
Naibu Waziri huyo amesema barabara hiyo ni sehemu ya barabara ya Mbalizi- Chang’ombe hadi Makongolosi yenye urefu wa kilometa 115 inayounganisha Mkoa wa Mbeya na Mkoa Songwe ambayo ujenzi wake unatekelezwa kwa awamu na mpaka sasa kilometa 10 zimekamilika na utekelezaji wake unaendelea.
Barabara ya Mbalizi-Chang’ombe-Mkwajuni Makongolosi inahudumia wananchi wa mikoa ya Songwe na Mbeya na ni muhimu kwa kukuza pato la taifa katika mikoa hiyo na inaunganisha Tanzania na nchi za za Zambia, Malawi na Msumbiji.