Benki ya CRDB imeingia makubaliano na kampuni ya mawasiliano ya Tigo Tanzania kuwawezesha wateja wa Tigopesa wanaokidhi vigezo vya kukopa kuanzia shilingi 500,000 mpaka shilingi milioni 2 kufanya hivyo kupitia huduma ya Tigo Nivushe iliyoboreshwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela na Mkurugenzi Mtendaji wa Tigopesa, Angelica Pesha

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye hafla ya kusaini mkataba huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema makubaliano hayo yanalenga kuwawezesha Watanzania kupata mkopo utakaowasaidia kufanikisha shughuli zao mahali popote walipo hivyo kuchangia kasi ya kukuza kipato cha mwananchi mmoja mmoja na uchumi wa taifa kwa ujumla.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tigopesa, Angelica Pesha amesema teknolojia imerahisisha kila kitu na idadi ya Watanzania wanaotumia simu za mkononi ambazo ni njia nzuri ya kuwafikishia huduma za fedha inazidi kuongezeka kia siku.