Watafiti wameonya juu ya hatari za kiafya zinazohusishwa na utumiaji mbaya wa dawa ya diazepam, maarufu kama Valium, baada ya utafiti kubaini kuwa dawa hiyo inauzwa kinyume cha sheria katika maduka ya dawa jijini.
Dawa hiyo ilipatikana katika asilimia 91 ya maduka ya dawa (178) ambayo yalihusishwa kwenye utafiti wilayani Kinondoni.
Asilimia 70 ya watoa dawa waliwauzia wateja bila kuona cheti cha daktari, licha ya kuwepo kwa sheria na kanuni za dawa zinazodhibiti utumiaji wa dawa hiyo.
Kinondoni, ilichaguliwa kwa ajili ya utafiti kutokana na kuwepo wa maduka mengi ya dawa, ikilinganishwa na maeneo mengi ya Tanzania.
Watafiti walijikita katika kufuatilia diazepam (tracer medicine) kwani ina uwezo mkubwa wakusababisha madhara makubwa kwa mtumiaji. Pia, inapatikana kwa urahisi katika maduka ya dawa.
“Ikitumiwa vibaya kwa muda mrefu [dawa hii] inaweza kuleta athari mbaya kama vile utegemezi na dalili ambazo zinaweza kuzidisha mashambulizi ya hofu, fadhaa, na matatizo ya kisaikolojia ya papo hapo,” watafiti waliandika.
Utafiti huo ulichapishwa katika Jarida la Utafiti wa Huduma za Afya wa BMC mwaka 2019 lakini matokeo yake bado yana maana hata leo, kwa mujibu wa mtafiti mkuu Wigilya Padili Mikomangwa, mfamasia katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).
Utoaji holela wa diazepam katika maduka ya dawa ya jamii unaweza kuwa unatokana na ukosefu wa usimamizi wa moja kwa moja wa wafamasia waliosajiliwa, watafiti wanasema.
Mikomangwa anasema ni wakati muafaka kwa mamlaka kuimarisha zaidi ufuatiliaji wa utoaji wa dawa zinazotakiwa kutolewa na daktari pekee.
“Ingawa utafiti [wetu] ulilenga dawa ya diazepam, matokeo yanaweza kuakisi mazoea katika utoaji wa dawa nyingine ambazo utoaji wake umedhibitiwa,” Mikomangwa ameliambia MwanaSayansi.
Zaidi ya miezi sita iliyopita, Msajili wa Baraza la Famasi Bibi Elizabeth Shekalaghe alitoa onyo kali kwa maduka ya dawa na wataalamu wa afya dhidi ya kutoa dawa zilizodhibitiwa. 178
Alizungumza katika mkutano mkuu wa mwaka wa Chama cha Wafamasia Tanzania, Juni 2021.
Hata hivyo, tangu utafiti huu ulipofanyika, jitihada mbalimbali zimechukuliwa ili kudhibiti utoaji holela wa dawa.
“Baraza la Famasi kwa mfano, sasa lina nia ya dhati ya kuhakikisha kuwa watoa dawa katika kila duka la dawa wanapata angalau diploma ya mafunzo ya famasi,” anasema Mikomangwa.
Wakati wa utafiti, mmoja wa watafiti alijifanya kuwa mtu mwenye ndugu anayehitaji diazepam, bila kuwa na cheti cha daktari. Hii inaelezea kwa nini taarifa kuhusu wanaotoa dawa kiholela hazikuweza kupatikana, mathalani viwango vyao vya elimu.
Chanzo: Utafiti.tz