WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema katika mwaka 2024/2025, Serikali imetenga kiasi cha sh. bilioni 787 kwa ajili ya kukopesha wanafunzi 250,000 wakiwemo 80,000 wa shahada ya kwanza ambao ni wapya.
“Maandalizi ya awali yameanza ikiwa ni pamoja na kusambaza mwongozo wa upangaji na utoaji mikopo; kufungua dirisha la uombaji mikopo kwa mwaka 2024/2025 kwa muda wa siku 90 kuanzia tarehe 1 Juni hadi 31 Agosti, 2024; kutoa elimu kwa waombaji mkopo na wadau wengine,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Juni 28, 2024) bungeni jijini Dodoma, wakati akitoa hotuba ya kuahirisha mkutano wa 15 Bunge. Bunge limeahirishwa hadi Agosti 27, mwaka huu.
Amesema katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali ilitoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu 224,056 na hadi kufikia Juni, 2024 wanafunzi hao walikuwa wamepatiwa mikopo yenye thamani ya sh. bilioni 743.2 sawa na asilimia 94.6 ya fedha zilizotengwa.
Mikopo hiyo ilitengwa kwa ajili ya wanafunzi wa ngazi ya stashahada, shahada ya awali, stashahada ya juu ya mafunzo ya Sheria kwa vitendo, shahada za umahiri na uzamivu, na ufadhili wa Samia (Samia Scholarships) katika masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati.
Kuhusu urejeshaji mikopo hiyo, Waziri Mkuu amesema Bodi ya Mikopo imeendelea kukusanya mikopo iliyoiva kutoka kwa wanufaika wa mikopo. “Kwa mwaka 2023/2024, Serikali ilipanga kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 230 ambapo hadi kufikia Mei 2024, shilingi bilioni 161 zilikusanywa sawa na asilimia 70 ya lengo.”
Ili kuimarisha ukusanyaji wa mikopo, Waziri Mkuu amesema Serikali imeweka mikakati kadhaa ikiwemo kuwakumbusha waajiri kuwasilisha majina ya wanufaika ndani ya siku 28 baada ya kuwaajiri; kushirikiana na kuunganisha mifumo na wadau wa kimkakati kama vile NIDA, TRA, taasisi binafsi za ndani na nje ya nchi; kufanya kampeni za kuwafichua wanufaika; kutoa elimu kupitia mitandao ya kijamii; na kufanya kaguzi kila mwezi kwa waajiri wa sekta ya umma na binafsi.
Katika hatua nyingine, akielezea utaratibu wa mikopo inayotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri, Waziri Mkuu amesema Serikali imekamilisha maandalizi ya uratibu wa upelekaji wa fedha za mikopo ya asilimia 10 katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwenda kwenye mfuko wa mikopo ya vikundi na kusimamia urejeshwaji wa mikopo iliyotolewa miaka ya nyuma.
“Itakumbukwa kwamba mwezi Aprili 2023, Serikali ilisitisha utoaji wa mikopo wa asilimia 10 kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu wa fedha 2023/2024, Serikali imekamilisha maandalizi ya uratibu wa upelekaji wa fedha za mikopo ya asilimia 10 katika mamlaka za serikali za mitaa kwenda kwenye mfuko wa mikopo ya vikundi na kusimamia urejeshwaji wa mikopo iliyotolewa miaka ya nyuma.”
Waziri Mkuu amesema katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali imepanga kutoa mikopo ya sh. bilioni 228 ambapo kati ya hizo, sh. bilioni 63.7 ni fedha za marejesho zilizokuwa zikiendelea kukusanywa kutokana na mikopo iliyotolewa kabla ya kusimamishwa Aprili, mwaka jana; sh. bilioni 63.2 ni fedha zilizokuwa zinatengwa kwa ajili ya mikopo na sh. bilioni 101.1 ni fedha ambazo zimetengwa kutokana na makisio ya makusanyo ya mapato ya ndani ya mwaka 2024/2025.
Akitoa ufafanuzi, Waziri Mkuu amesema Serikali imepanga utaratibu wa kutumia benki kwa Halmashauri 10 za majaribio ambazo ni Majiji ya Dar es Salaam na Dodoma, Manispaa za Kigoma Ujiji na Songea, Miji ya Newala na Mbulu, Wilaya za Siha, Nkasi, Itilima na Bumbuli.
Amesema, halmashauri 174 zilizobaki zitatumia utaratibu ulioboreshwa ikiwemo uanzishwaji wa kitengo cha usimamizi wa mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika Ofisi ya Rais – TAMISEMI, na uanzishwaji wa kamati za usimamizi wa mikopo katika ngazi za Ofisi za Wakuu wa Wilaya, Halmashauri na Kata.