WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imesaini mkataba wa sh. bilioni 346 na Benki ya Dunia kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi ambao unalenga kuimarisha usalama wa milki za ardhi na kuwezesha miundombinu ya usimamizi wa ardhi nchini.

Shamba

Amesema mkataba huo uliosainiwa Februari, 2022 ni wa mradi ambao unatekelezwa kwa miaka mitano (2022/2023 – 2026/2027) katika Halmashauri 67 na Mikoa 26. Mradi huo una vipengele vinne ambavyo ni kuongeza usalama wa milki za ardhi kwa njia ya urasimishaji kwa kutoa Hatimiliki 1,000,000 katika maeneo ya mijini na Hatimiliki za Kimila 500,000; kuimarisha mifumo ya taarifa za ardhi; kujenga miundombinu ya ardhi; na usimamizi wa mradi.

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Ijumaa, Juni 28, 2024) wakati akitoa hotuba ya kuahirisha mkutano wa 15 wa Bunge jijini Dodoma.  Bunge limeahirishwa hadi Agosti 27, mwaka huu.

Akielezea mradi huo, Waziri Mkuu amesema hadi kufikia Juni 15, mwaka huu, kazi zilizotekelezwa ni pamoja na urasimishaji wa vipande vya ardhi 62,200 katika Halmashauri mbalimbali; usimikaji wa alama za msingi za upimaji 327 katika Halmashauri 26; upimaji, uhakiki mipaka ya vijiji na uandaaji wa Vyeti vya Ardhi ya Vijiji 843 katika Halmashauri 21; uandaaji wa Hatimiliki za Kimila 381,509.

“Mradi umewezesha kununuliwa magari 18 ambayo yanatumika kwenye maeneo mbalimbali nchini na taratibu za ununuzi wa magari mengine 52 zinaendelea na yanatarajiwa kuwasili Septemba, 2024. Hatua hii itapunguza changamoto kubwa ya usafiri iliyopo katika sekta ya ardhi,” amesema.

Waziri Mkuu amezitaka Mamlaka za Upangaji Miji chini ya Uratibu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ziendeleze kasi ya utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi kwa ufanisi ili fedha zilizopangwa kutumika kwenye mradi huo ziwe na tija.

Amezitaka pia, zipunguze migogoro kupitia uhakiki na upimaji wa mipaka ya vijiji; Maandalizi ya mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji; kuandaa Mipangokina ya vijiji na kuandaa Hati za Hakimiliki za Kimila; kurasimisha vipande vya ardhi; kubadilisha nyaraka za ardhi kutoka analojia kwenda kidijitali; na kusanifu na kusimika vituo vya kieletroniki vya upimaji. “Nitoe wito kwa wananchi, hususan wa maeneo ya vijijini kuchangamkia fursa ya uwepo wa mradi huo kwa kurasimisha maeneo yao.”

Kuhusu malipo ya fidia ya ardhi kwenye maeneo yanayotwaliwa na Serikali kwa ajili ya uwekezaji, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kutwaa maeneo hayo kwa ajili ya miradi yenye manufaa ya umma ikiwemo ujenzi wa barabara, viwanja vya ndege na uchimbaji wa madini.

“Serikali inatambua kuwa kwa nyakati tofauti kumekuwepo na malalamiko ya wananchi kucheleweshewa malipo ya fidia katika baadhi ya maeneo. Katika kuhakikisha kuwa malalamiko haya yanatatuliwa, nazielekeza taasisi zote zihakikishe kuwa zinatenga fedha katika bajeti zao kwa ajili ya kulipa fidia kabla ya kuanza zoezi la utwaaji kama inavyoelekezwa katika Waraka wa Uthamini na Fidia Na. 1 wa mwaka 2024,” amesisitiza.