Kwa miaka mingi, homa ya dengue, ambayo huenezwa na mbu, imekuwa ikidhibitiwa  kwa mipango ya muda mfupi nchini Tanzania. Hatua zinachukuliwa tu wakati wa milipuko. Hata hivyo, malaria, ambayo pia huenezwa na mbu, imekuwa ikishughulikiwa kwa mipango ya muda mrefu na iliyo imara. Katika utafiti mpya, watafiti nchini Tanzania wamependekeza kuwa hatua za kudhibiti dengue zijumuishwe kwenye mipango na programu za kitaifa za kudhibiti malaria.

Utafiti uliochapishwa Machi 2024 katika Jarida la Kitabibu la Tanzania, yaani Tanzania Medical Journal (TMJ) una onyesha umuhimu wa dengue kujumuishwa katika programu zilizopo kama vile za udhibiti wa malaria.

Watafiti wanasema njia hii inaweza kurahisisha upatikanaji wa rasilimali fedha za kuzuia magonjwa yote mawili kwa gharama nafuu na kuongeza uwezekano wa kuokoa maisha ya watu zaidi nchini Tanzania.

Zaidi ya watu 6,800 walipata maambukizi ya virusi vya dengue na  vifo 13 vilirekodiwa wakati wa mlipuko wa mwisho wa dengue nchini Tanzania mnamo mwaka 2019. Mwaka mmoja baada ya mlipuko huo, watafiti walichunguza jinsi Mpango wa Udhibiti wa Malaria wa Tanzania unavyoweza kutumika pia kupambana na dengue.

Watafiti waligundua kuwa udhibiti wa dengue unaweza kujumuishwa kwenye programu za malaria, lakini walibaini changamoto, mathalani utashi wa kisiasa kwa upande wa serikali, hofu kwamba njia hii inaweza kuongeza gharama za ziada na ikawa mzigo kwa wataalmu wa afya, pia kulikuwa na swala la vipaumbele tofauti vya wafadhili. Dengue inachukuliwa kama  miongoni mwa magonjwa wa Kitropiki  yasiyopewa kipaumbele (NTDs) nchini Tanzania. Hii inamaanisha kuwa haina mpango maalum wa kitaifa.

“Tukifanya maamuzi ya kujumuisha udhibiti wa dengue katika programu za kudhibiti malaria, nchi inaweza kujenga mfumo wenye ufanisi zaidi na ufanisi wa kulinda afya ya umma,” anasema mtafiti kiongozi wa utafiti huo, Dorice Lymo, mtaalamu wa usimamizi wa afya na Katibu wa Afya wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha.

Lymo, akishirikiana na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), walifanya mahojiano na maafisa 15 kutoka Mpango wa Kitaifa wa Kudhibiti Malaria (NMCP) wa Wizara ya Afya, na mpango wa Magonjwa ya Kitropiki Yasiyopewa kipaumbele (NTDs). Waligundua kuna utayari miongoni mwa  watumishi katika taasisi hizo.

“…Wengi wao walionyesha nia ya kubeba mzigo wa ziada [wa dengue], na miundombinu iliyopo inaweza kutumika kwa magonjwa yote mawili,” anasema Lymo. Mwa mujibu wa utafiti huo, wadau waliohojiwa walionekana kukubaliana na njia hiyo ya udhibiti.

“…Mbu wa Aedes bado wapo katika jamii zetu na wanasambaza virusi vinavyosababisha homa ya dengue. Hii inamaanisha kuwa hatua zetu dhidi ya mbu huyu wa dengue zinapaswa kuwa za muda mrefu,” anasema Lymo, na kuongeza: “Kwa matokeo haya, hoja yetu mauhususi ni kwamba tufungamanishe udhibiti wa magonjwa haya yanayoenezwa na mbu nchini Tanzania.”

Hatahivyo, watafiti walibaini kuna hofu juu ya gharama za uendeshaji miongoni mwa waliohojiwa na hili walilitilia maanani kama jambo la msingi na hivyo wanapendekeza kuwepo kwa ushirikiano baina ya idara mbalimbali za serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali ili kutatua changamoto za gharama zinazoweza kujitokeza.

Kwasababu za  upungufu wa rasilimali watu na fedha kwenye sekta ya umma, Shirika la Afya Duniani (WHO) linapendekeza usimamizi jumuishi wa magonjwa kama haya ili kuziwezesha nchi kukabiliana vyema na changamoto zitokanazo na kudhibiti magonjwa yanayo enezwa na wadudu, kama mbu hawa.

Mtafiti mwenza wa utafiti huo, Dkt. Nathanael Sirili, ambaye ni mhadhiri mwandamizi na mtafiti wa mifumo ya afya kutoka MUHAS, anasema kuwa ugonjwa wa dengue ukiendelea kuwekwa katika kundi la magonjwa yasiyopewa kipaumbele, utaendelea kutodhibitiwa inavyotakiwa na utazidi kuleta madhara.

“Dengue mara nyingi imewekwa katika kundi la magonjwa yasiyopewa kipaumbele kutokana na viwango vya chini vya vifo vinavyo husiana ugonjwa huo. Hata hivyo, mwanafamilia akipoteza maisha kutokana na dengue, inakuwa ni hasara ya asilimia 100 kwa familia,” anasema Dkt.

“Huu ugonjwa ukiwekwa kwenye udhibiti jumuishi na malaria, njia hii itaruhusu matumizi ya rasilimali chache lakini kutaleta matokeo makubwa zaidi. Hakuna haja ya kuwa na programu mbili. Kuwa na programu mbili tofauti ( ya dengue na malaria) inamaanisha kuwa inabidi kutenga rasilimali kwa ajili ya dengue na nyingine kwa ajili ya malaria.”

Jinsi ya kupata utafiti huu:

Tanzania Medical Journal(TMJ): Organizational Facilitators

and Barriers for the Integration of Dengue into The National Malaria Control

Program in Tanzania: A Case Study