Na Derek Murusuri, Dodoma.

Waandishi nchini wametakiwa kulisaidia taifa kwa kufanya tafiti zitakazoisaidia Serikali kutoa maamuzi ya kuiendeleza nchi na kutumia tafiti zao kuielimisha jamii.

“Vyombo vya habari havijalisaidia sana Taifa kwani vinatoa habari lakini havitoi elimu,” alisisitiza.

Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais Mstaafu, Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba, aliyasema hayo wakati akifungua Kongamano la MCT la wadau wa Habari na uchaguzi Tanzania.

Alisema kuwa vyombo vya habari vinaandika na kutangaza habari za matukio zaidi pasipo kuzingatia mojawapo ya misingi yake mikuu mitatu, msingi wa kuelimisha.

Jaji Warioba alisisitiza umuhimu wa vyombo vya habari kufanya utafiti na kuielimisha jamii na kuishauri Serikali kuhusu matokeo ya tafiti hizo.

Amewataka wanahabari wasiwe sehemu ya kulalamika (reactive) wakati wanayo nafasi ya kutengeneza agenda (activation) kwa kufanya utafiti na kutoa elimu ya mambo ya msingi kwa nchi.

Kongamano hili lilipokea salamu za Serikali kutoka kwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Tanzania (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi.

Katika nasaha zake, kwa washiriki wa Kongamano hilo la Wadau wa Habari, Ndg Matinyi ameipongeza MCT kwa kuandaa Kongamano hilo na  mchango wake katika kuboresha weledi, maadili na uwajibikaji kwenye tasnia ya habari.

Alisema MCT imesaidia katika kuboresha viwango vya kazi za uandishi na utangazaji wa habari nchini, ikiwa ni pamoja na kutetea haki za wananchi pamoja na waandishi wa habari. 

Msemaji huyo Mkuu wa Serikali, pia amevishukuru vyombo vya habari kwa kazi kubwa na nyeti wanayoifanya ya kuuelimisha umma, hasa katika kipindi cha Uchaguzi.

Hata hivyo, amevikumbusha vyombo hivyo nchini kuzingatia uandishi wa habari za kweli, zilizo sahihi na zinazozingatia mizania. 

Alionya kuwa uandishi na usambazaji wa habari za uongo si tu zinahafifisha taswira ya nchi na ya fani ya uandishi wa habari, bali pia zinahafifisha taswira ya mwandishi na vyombo vyao.

Mapema, akielezea madhumuni ya Kongamano hilo,  Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ndg. Ernest Sungura pia amesema kuwavyombo vya Habari vya Tanzania huwa havina maandalizi ya Pamoja ya namna ya kuandika na kutangaza Habari za uchaguzi.

“Havina maandalizi katika kila hatua ya mchakato wa uchaguzi kuanzia uboreshaji wa daftari la wapiga kura, kujiandikisha kwa wapiga kura, uteuzi wa wagombea, elimu kwa mpiga kura na kampeni hadi siku ya kupiga kura,” alisema.

Alibainisha kuwa vyombo vya Habari vya Tanzania huwa vinajikita katika maneno ya wanasiasa na mambo binafsi ya wagombea badala ya kujikita katika kuelimisha na kutoa taarifa sahihi za masuala ya msingi na mambo yanayowaathiri wananchi katika Maisha yao ya kila siku.

Ndg Sungura aliongeza kwamba, vyombo vya Habari vya Tanzania huwa havina uelewa mpana wa viwango vya kimataifa vya masuala ya uchaguzi, sheria na kanuni mbalimbali za uchaguzi Tanzania.

“Mambo mengine ni pamoja na mifumo ya usimamizi wa uchaguzi  Tanzania, uelewa mpana wa sera, itikadi ya vyama vya siasa na ilani zao za uchaguzi,” alimalizia.

Kauli mbiu ya kongamano hilo la wadau wa Habari na Uchaguzi Tanzania ni Uandishi wa Habari za Uchaguzi kwa Weledi Hujenga USAWA, HAKI na UWAJIBIKAJI.

Naye Katibu ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Ndg Amos Makalla, amesema CCM itakuwa mstari wa mbele katika kutekeleza kwa vitendo haki, usawa na wajibu ili kuwa na uchaguzi ulio huru, wa haki na wenye kuaminika.

Ndg Makalla alimwakilisha Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi.

Makalla alivikumbusha vyombo vya habari kuwa, pamoja na kuandika habari zao kwa uhuru, wanapaswa kutambua kuwa hatuna nchi mbadala, hivyo ilikuwa muhimu kuhakikisha kuwa habari zote  zinaiacha nchi ikiwa salama na yenye amani.

Kongamano hilo vilevile limehutubiwa na Wawakilishi wa Balozi za Uingereza na Marekani.