Tanzania na China zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja kwa kuyawezesha Makampuni ya Tanzania kupewa sehemu ya kazi za ujenzi kutoka kwa Makampuni ya Kichina yatakayopewa kazi ya kutekeleza miradi ya ujenzi nchini.
Makubaliano hayo yamefikiwa leo Mei 20, 2024 jijini Dar es Salaam wakati wa Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa pamoja na Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian walipokutana na kufanya mazungumzo kuhusu ushirikiano wa masuala mbalimbali katika Sekta ya Ujenzi baina ya nchi hizo mbili.
Bashungwa ameeleza kuwa ushirikiano huo utakuwa katika maboresho ya vipengele vya zabuni na mikataba ya ujenzi itakayosainiwa ambapo itakuwa ni moja ya mkakati wa Serikali wa kuongeza ushiriki wa Makandarasi na Washauri Elekezi Wazawa kwenye utekelezaji wa miradi.
Aidha, Waziri Bashungwa amejadiliana na Balozi Mingjian juu ya baadhi ya kampuni za Makandarasi za China zinazotekeleza miradi kwa kusuasua na kuzitaja kampuni mbili ambazo ni China Railway Seventh Group (CRSG) na STECOL Corporation na ameeleza kuwa tayari hatua mbalimbali za kimkataba zimeanza kuchukuliwa.
Kwa upande wake, Balozi wa China nchini, Mhe. Chen Mingjian ameeleza jinsi China inavyouthamini ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na China na kumuahidi Waziri Bashungwa kuendelea kutoa fursa kwa Makandarasi wazawa katika utekelezaji wa miradi nchini.
Amefafanua kuwa Tanzania na China ina zaidi ya miaka sitini ya ushirikiano wa kidiplomasia ambao umeleta mapinduzi ya kimaendeleo, hivyo wanao wajibu wa kuendeleza ushirikiano huo ili kukuza uchumi wa mataifa hayo katika Siasa, Uchumi na Utamaduni.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Ujenzi na Ubalozi wa China nchini Tanzania wakiongozwa na Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Mhandisi Aloyce Matei ambaye ni Mkurugenzi wa Barabara pamoja na timu ya watalaam kutoka kwa Wakala wa Barabara (TANROADS) wakiongozwa na Mtendaji Mkuu Mhandisi Mohamed Besta.