WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema michezo ni zaidi ya afya na burudani, ni fursa ya ajira na pia hupunguza magonjwa mwilini.
“Kama mnavyofahamu, michezo ni zaidi ya afya na burudani lakini leo tunathibitisha kuwa baada ya mbio hizi, sote tumefurahi na miili yetu imeimarika.”
Ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Mei 11, 2024) wakati akizungumza na viongozi, wananchi na washiriki waliohudhuria hafla ya kufunga hafla ya TULIA MARATHON iliyofanyika kwenye uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.
Amesema kwa mujibu wa Wizara ya Afya, michezo inawezesha watu kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza. “Taarifa za Wizara zinasema kuwa nchi yetu inakabiliwa na changamoto ya ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza kama vile shinikizo la damu, kisukari, kiharusi na maumivu ya viungo kama magoti na mgongo. Kwa hiyo tujenge tabia ya kufanya mazoezi, ” amesema.
Amesema hivi sasa fedha nyingi zinatumika kutibu maginjwa hayo iwe ni kwa Serikali au mtu mmoja mmoja na kwamba magonjwa hayo yanaendelea kupoteza nguvukazi ya Taifa.
Ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuboresha michezo na hivyo kuongeza hamasa ya kitaifa ya kupenda michezo. “Sote tunakumbuka kuwa alianzisha mpango wa goli la Mama, akaanzisha changizo la Kitaifa kwa ajili ya timu za Kitaifa na hii inaenda sambamba na michezo ijayo ya AFCON 2027.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii izitumie mbio za Tulia Marathon kutangaza utalii wa mkoa wa Mbeya na mikoa iliyo jirani. “Mkoa huu una vivutio vingi na mikoa ya jirani inavyo vivutio mbalimbali. Tumieni mbio hizi kuwa fursa ya kutangaza utalii. TANAPA wekeni banda hapa, onesheni kuna vivutio gani kwenye mkoa huu na mikoa ya jirani,” amesema.
Pia amewataka wafanyabiashara na wakulima wa mkoa huo na mikoa jirani watumie mbio hizo kama jukwaa la kutangaza biashara zao na kupata masoko. Aidha, amemtaka Mkuu wa Mkoa huo, na Wakuu wa Wilaya waipe ushirikiano taasisi hiyo kwa vile imesambaa mkoa mzima na inatoa huduma kwa wakazi wote wa mkoa huo.
Waziri Mkuu pia ameitaka taasisi ta Tulia Trust ione umuhimu wa kupanua mbio hizo ili kujumuisha pia washiriki kutoka nchi nyingi zaidi za jirani. “Natambua kuwa sasa hivi kuan washiriki kutoka Kenya na Uganda, ni vema sasa uongozi wa Tulia Trust, ukaona namna ya kupanua mialiko hadi nchi jirani za Malawi, Zambia, Congo na Msumbiji ili zipande hadhi na kuwa za Kimataifa.”
Waziri Mkuu alikabidhi medali na zawadi za fedha taslimu kwa washindi wa kwanza hadi wa tatu wa mbio za km. 10, km. 21 na km. 42.
Mapema, Spika na Rais wa Mabunge ya Dunia (IPU), Dkt. Tulia Ackson ambaye pia ni muasisi wa mbio hizo, alisema taasisi ya Tulia Trust ilikuwa ikijielekeza kutatua changamoto za miundombinu ya elimu na afya lakini sasa inalènga kuja na kitu kipya kwa sababu hivyo vyote vinafanywa na Serikali ya awamu ya sita.
“Tunahitaji kupata ekari 15 za kujenga kituo cha kukuza vipaji vya vijana wanaopenda riadha. Tunataraji kuanza ujenzi huo mwaka huu, na kikikamilika, kituo hicho kitakuwa kinatumiwa na watu kutoka nchi nzima na nje ya nchi,” alisema.
Alisema miaka ya nyuma walikuwa wakinunua madawati, madaftari ya wanafunzi na kujenga madarasa, mabweni, pamoja na kusaidia kwenye huduma za afya lakini kwa sasa Serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya miundombinu hiyo.
Naye, Dkt. Joyce Komba kutoka hospitali ya Rufaa ya Mbeya alisisitiza umuhimu wa wananchi kufanya mazoezi kila mara ili kuboresha afya na kupunguza changamoto ya magonjwa yasiyoambukiza.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu alimkabidhi Bibi Maligo Diamond nyumba ya vyumba vitatu ambayo imejengwa na taasisi ya Tulia Trust ili kumsaidia kutoka kwenye changamoto ya maisha duni na kumwezesha aishi maisha bora yeye na familia yake.