WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watendaji wote wanaohusika na sera na mipango katika Serikali Kuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa wahakikishe kuwa mipango na maamuzi yote yanayohusu maendeleo ikiwemo utoaji wa huduma kwa wananchi yanazingatia matokeo ya Sensa ya mwaka 2022.
Amesema hayo jana (Jumamosi, Juni 22, 2024) wakati wa hafla ya uzinduzi ripoti ya Kidemografia, Kijamii, Kiuchumi na Mazingira zinazotokana na Sensa ya Watu na Makazi na Sensa ya Majengo ya Mwaka 2022. Hafla hiyo imefanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es salaam.
Amesema kuwa matokeo hayo ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa kwa kuwa yanatoa fursa kwa nchi kuendelea kutambua kwa kina hali za kidemografia, kiuchumi, kijamii na mazingira pamoja na hali ya makazi. “Ripoti hizi zina mchango mkubwa katika kutunga na kuhuisha sera mbalimbali zinazohusiana na masuala ya ustawi wa wananchi ikiwemo uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.”
Waziri Mkuu amesema kwa upande wa sekta ya nishati, matumizi ya nishati safi kwa ajili ya kupikia yameongezeka hapa nchini ambapo, kaya zinazotumia umeme kwa ajili ya kupikia zimeongezeka kutoka asilimia 1.6 mwaka 2012 hadi asilimia 4.3 mwaka 2022 na gesi kutoka asilimia 0.9 mwaka 2012 hadi asilimia 9.4 mwaka 2022.
Amesema kuwa Serikali inasisitiza kuwa matokeo ya Sensa yatumike kikamilifu katika kubaini na kutatua changamoto zinazoikabili jamii kwa namna ambayo ni endelevu. “Nirudie kusisitiza kuhusu umuhimu wa matumizi ya matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi katika ngazi zote za utawala wakati tunapopanga mipango na programu za maendeleo ya wananchi”.
Ameongeza kuwa kupitia utekelezaji wa Sensa ya kidijitali ya Watu na Makazi, Sensa ya Majengo na Sensa ya Anwani za Makazi ya Mwaka 2022, Tanzania imetoa mchango wa uzoefu wake katika kufanikisha sensa za nchi nyingine Kikanda na Kimataifa.
“Kimataifa Tanzania imeshaalikwa mara kadhaa na Umoja wa Mataifa kutoa uzoefuwake katika utekelezaji wa Sensa ya kidijitalikatika kuzisaidia nchi nyingine ambazo zilikuwa zinajiandaa kufanya Sensa zao katika Mzunguko wa miaka ya 2020 ya Umoja wa Mataifa wa Kufanya Sensa, ambao ulianza mwaka 2015 na utaisha mwaka 2024.”
Kwa upande wake, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar na Mwenyekiti Mwenza wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla (MBM) alisemaSensa ya watu na makazi ya 2022 ikifanywa na JMT chini ya Samia na Mwinyi imekuwa Sensa ya Mfano hivyo hivyo wataalam wafanye tafsiri ya takwimu za Sensa kwa maslahi ya taifa letu.
Awali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo, akiongea kwa Niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama, alimshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa maono yao na miongozo thabiti iliyopelekea kukamilisha kwa ufanisi zoezi la Sensa ya Watu na Makazi pamoja na Sensa ya Majengo ya mwaka 2022.
Aidha, aliongeza kusema kuwa, kutokana na kufanikiwa kwa zoezi hilo muhimu, viongozi hawa wameendelea kuliongoza Taifa katika mipango na mikakati mbalimbali ya maendeleo kwa kutumia vizuri Takwimu hizo za Sensa ya Watu na Makazi na matokea chanya yanaendelea kuonekana.
Pia, Dkt. Jafo alizipongeza Ofisi mbili za Takwimu kwa kazi nzuri waliyoifanya kuanzia wakati wa maandalizi ya zoezi la Sensa ya Watu na Makazi, 2022 hadi ukamilifu wake. “Ofisi hizi zimefanya kazi kubwa ya uaandaaji wa nyaraka zinazoonyesha takwimu ya makundi mbalimbali kutokana na matokeo ya Sensa.