Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati wa Tanzania, Mhe. Dkt. Doto Biteko
amefungua rasmi maonesho ya Wiki ya Nishati katika Viwanja vya Bunge
jijini Dodoma ambapo amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa
kuimarisha  Sekta ya Nishati  kutokana na nyenzo na maelekezo
anayoyatoa ambayo yamempambanua kama kiongozi anayetatua matatizo ya
wananchi kwa kutenda zaidi na si kusema.

Dkt. Biteko ameeleza kuwa, maelekezo  ya Rais, Dkt. Samia pamoja na
nyenzo anazozitoa kwa Wizara ya Nishati zimepelekea nchi sasa kuwa na
umeme wa kutosha na kwamba  hakuna mgawo tena huku kukiwa na mitambo
ambayo ipo standby kuwashwa pale inapotokea hitilafu kwenye mitambo
mingine ya uzalishaji umeme.

Aidha, kwa mikoa ambayo ipo nje ya gridi ya Taifa ikiwemo Katavi,
Rukwa, Kigoma, Lindi na Mtwara, amesema kuwa yote itaunganishwa kwenye
gridi ya Taifa kwani Rais, Dkt. Samia ameshatoa fedha za kutekeleza
miradi ya umeme itakayoiunganisha mikoa hiyo na gridi ambayo tayari
inaendelea.

Katika hatua nyingine,  Dkt. Biteko ameipongeza TANESCO kwa kuendelea
kuimarisha utendaji kazi wao ikiwemo utatuzi wa changamoto za umeme
akitolea mfano athari iliyotokea katika gridi ya umeme usiku wa siku
ya Pasaka kutokana na hitilafu kwenye mfumo wa kudhibiti kiwango cha
maji kwenye mitambo ya Kidatu ambapo tatizo hilo lilipaswa
kushughulikiwa kwa siku tatu lakini TANESCO ilifanya jitihada na
kutatua changamoto hiyo kwa muda wa masaa kadhaa.

Pamoja na pongezi  hizo Dkt. Biteko ametoa angalizo kwa kampuni tanzu
za TANESCO  kuhusu utendaji kazi wao ikiwemo Kampuni ya Uendelezaji wa
Jotoardhi Tanzania (TGDC) ambapo kampuni hiyo ilitoa ahadi ya kuanza
uchorongaji wa visima vya Jotoardhi katika eneo la Ngozi Mbeya tarehe
1 Aprili 2024 lakini bado hawajaanza kazi hiyo  hivyo amemuagiza
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati kuisimamia ipasavyo kampuni hiyo ili
nchi iweze kupata umeme wa Jeothemo.

Pamoja na uendelezaji wa Sekta ya Umeme, Dkt. Biteko amesema kuwa
Wizara inaendelea na utekelezaji wa mipango mingine ikiwemo wa nishati
safi ya kupikia ambapo Baraza la Mawaziri limeshapitisha Mpango
Mkakati wa Nishati safi ya kupikia na sasa kinachofanyika ni
utekelezaji ili asilimia 80 ya wananchi watumie nishati safi ya
kupikia ifikapo mwaka 2033.

Katika Sekta ndogo ya Gesi Asilia amesema kuwa, usimamizi madhubuti
unaendelea ambapo chini ya Serikali ya Awamu ua Sita, imetolewa leseni
ya uchimbaji wa Gesi asilia katika kisima cha Ntorya mkoani Mtwara
huku leseni ya mwisho ikiwa imetolewa mwaka 2006.

Kuhusu Maonesho ya Wiki ya Nishati,  Dkt. Biteko amewaagiza Wataalam
kuwa, pamoja na kueleza utekelezaji wa mipango ya Serikali na mipango
mipya iliyopo lakini wanapaswa kutatua na kujibu hoja mbalimbali za
Wananchi na Wabunge na si kuzichukua ili kuyapa thamani maonesho hayo.

Vilevile, amewapongeza Wabunge wote kwa usimamizi wa karibu wa Sekta
ya Nishati na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi mbalimbali
pamoja na utatuzi wa kero zinazowahusu wananchi.

 Kwa upande wake, Naibu Spika wa Bunge. Mhe. Mussa Zungu amepongeza
Wizara ya Nishati na Taasisi zake kwa Maonesho hayo hususan matumizi
ya teknolojia ya kisasa katika kuhifadhi taarifa mbalimbali ikiwemo
taarifa za maeneo yenye umeme, yasiyo na umeme, mfumo wa gridi n.k
suala linalowezesha taarifa hizo kupatikana kwa urahisi na kwa haraka
pale zinapohitajika.

Ameeleza kuwa, Bunge litaendelea kufanya kazi kwa karibu na Serikali
na kuhakikisha fedha za kutekeleza miradi mbalimbali zinapatikana .

Pia amempongeza Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza ahadi yake
ya uwepo wa umeme wa uhakika nchini kwani suala hilo sasa limeonekana
kwa vitendo na malalamiko ya wananchi kuhusu changamoto za umeme
yamepungua na pia kwa nia dhati ya kuamua kumtua mama kuni kichwani
kwa kutekeleza ajenda ya nishati safi ya kupikia.

Viongozi mbalimbali walioambatana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati katika uzinduzi huo ni  Waziri wa Nchi, Sera, Bunge na
Uratibu, Mhe. Jenista Mhagama, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith
Kapinga, Wenyeviti wa Kamati mbalimbali za Bunge, Wajumbe wa Kamati
mbalimbali za Bunge na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi
Felchesmi Mramba.