Kamamti ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeipongeza Wizara ya Ujenzi kwa kuandaa andiko la mkakati wa kuwawezesha makandarasi wazawa na washauri elekezi kwenye utekelezaji wa miradi ya Ujenzi na kusisitiza andiko hilo kushirikisha wataalamu kutoka Sekta mbalimbali nchini ili kuweza kuleta tija kwa Taifa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC),
Mheshimiwa, Naghenjwa Kaboyoka, akisisitiza jambo wakati akitoa maoni yake kuhusu
mkakati wa kuongeza ushiriki wa wazawa kwenye miradi ya Ujenzi nchini iliyoandaliwa
na Wizara ya Ujenzi, jijini Dodoma.

Akizungumza katika Semina iliyofanyika jijini Dodoma Aprili 9, 2024 Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Mheshimiwa, Naghenjwa Kaboyoka, pamoja na mambo mengine amesisitiza ni muhimu kwa Wizara kupata maoni kutoka kwa wahandisi, wakandarasi, wachumi na wataalam kutoka Wizara ya Fedha ili kuona namna ya kuboresha wazo hilo.

“Tunawapongeza Wizara ya Ujenzi kwa kuja na wazo hili, wazo ni zuri na tumelipokea, maoni mliopewa na waheshimiwa wabunge hakikisheni mnayafanyia kazi na mpange tena semina nyingine ya kushirikisha wadau wote ili kupata maoni zaidi”, amesema Kaboyoka.

Aidha, amefafanua kuwa moja ya mapendekezo yanayotakiwa kufanyika ni pamoja na maboresho katika Sera ya Ujenzi na mabadiliko ya Sheria ambazo zinamnyonya mkandarasi wa ndani na kuhakikisha wataalam hao wanajengewa uwezo kwa kupatiwa fursa ya kutekeleza miradi midogo na mikubwa.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mha. Godfrey Kasekenya ameishukuru Kamati ya PAC kwa kuendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha kuwa ushiriki wa Makandarasi na Wahandisi Washauri Wazawa unasimamiwa kikamilifu kwa ukuaji wa uchumi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

Kadhalika, Kasekenya ameeleza kuwa Tathmini iliyofanyika ilibaini kuwa wazawa walitekeleza miradi 35,351 yenye thamani ya shilingi Trilioni 23.749 sawa na asilimia 38.5 ya jumla ya thamani ya miradi yote 36, 839 yenye thamani ya Shilingi Triloni 61.638 iliyosajiliwa katika kipindi cha kuanzia 2013 hadi 2023.

“Ni Dhahiri kwamba ingawa wazawa wametekeleza miradi mingi kwa idadi, lakini miradi hiyo ina thamani ndogo kuliko miradi michache iliyotekelezwa na wageni, hali hii haikubaliki, ni lazima tufanye mikakati ya haraka kuwainua wazawa”, amesema Kasekenya.

Naye, Muwasilishaji wa andiko hilo, abaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Baraza la Taifa la Ujenzi, Dkt. Matiko Nturi, amesema kuwa utafiti uliofanyika   umeonesha masuala mbalimbali ikiwemo wazawa kukosa uzoefu wa utekelezaji wa miradi mikubwa, uwezo wa kifedha au mitaji ya kutosheleza kutekeleza miradi, kutokuwa na mitambo ya uhakika pamoja na wataalam wa kutosha wenye uzoefu na hivyo wengi kushindwa kukidhi vigezo vya zabuni.