Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema  Viongozi na Watanzania wanajifunza mengi  kutokana na historia ya utendaji kazi  wa Mzee John Samwel Malecela  katika nyadhifa mbalimbali alizoshika Serikalini na Chama cha Mapinduzi na ataendelea kuwa hazina  muhimu  ya maarifa na uzalendo hapa nchini.

Rais Dk.Mwinyi amesema hayo katika sherehe za Kumbukizi ya  miaka 90 ya kuzaliwa Mhe.Mzee John Samwel Malecela, Waziri Mkuu na Makamu wa Rais  Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyofanyika nyumbani kwake Uzunguni Jijini Dodoma tarehe:21 Aprili 2024.

Aidha Rais Dk.Mwinyi amempongeza Mzee John Samwel Malecela kwa kutimiza umri huo na amemuomba Mwenyezi Mungu aendelee kumjalia umri mrefu na afya njema.

Rais Dk.Mwinyi ameeleza kuwa Watanzania  wataendelea kufaidika na busara, hekima, na ushauri wake katika kuiletea maendeleo nchi yetu na uzoefu wake mkubwa alionao Mzee Malecela katika uongozi, siasa na diplomasia ya Kimataifa.

Viongozi mbalimbali wa Serikali, Chama cha  Mapinduzi  na Dini Wamehudhuria akiwemo Waziri Mkuu Mstaafu Mhe.Cleopa Msuya, Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye, Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara Comrade Abdulrahman Kinana, Spika wa Bunge Mstaafu Mhe.Job Ndugai, Mkuu wa Mkoa  wa Dodoma Mhe.Rosemary Senyamule, Mwenyekiti wa UWT Taifa Ndugu Mary Chatanda.