Waandishi Wachangiaji: Juliana Mutagaywa na Samora Lupalla
Ili kukabiliana na mahitaji mbalimbali ya fedha, wakaazi wa vijijini hususani wanawake na vijana, hulazimika kukabiliana na mahitaji hayo kwa kutumia huduma (nyenzo) mbalimbali za fedha na zisizo za fedha. Huduma (nyenzo) za kawaida za fedha ambazo hutumiwa katika kaya za vijijini, hasa kwa akiba na mikopo, ni Vikundi vya Kijamii vya Huduma Ndogo za Fedha (CMG).
Utafiti wa Finscope Tanzania 2017 unaonyesha kuwa 17% na 18% ya kaya za Tanzania hutumia Vikundi (CMGs) kuweka akiba na kukopa mtawalia.
Zuhura ni mama mjane mwenye umri wa miaka 48 mama wa watoto wanne (4). Anaishi kijijini, na kiwango chake cha elimu ni shule ya msingi (Darasa la 7). Anaishi kwa kipato kinachotokana na kuuza bidhaa za kilimo. Miongoni mwa changamoto anazokabiliana nazo katika kuwalea watoto wake wanne ni kutokuwa na kipato cha kutosha kukidhi gharama za kaya yake yaani za, chakula, mavazi, elimu na afya. Hatumii huduma rasmi za fedha kwa sababu anadhani kuwa hakidhi vigezo vya kutumia huduma kama hizo.
Zuhura pia anadhani kwamba taasisi za fedha kama vile benki zipo kwa ajili ya kuwahudumia matajiri na watu wenye vipato vikubwa, na kwa sababu hiyo hajawahi kwenda benki. Badala yake, anakopa pesa kutoka kwa marafiki, familia/ndugu, pamoja na wakopeshaji fedha binafsi.
Zuhura kisha anahifadhi fedha ambazo anaweza kulimbikiza kutoka kwenye biashara zake nyumbani.
Changamoto anazokumbana nazo Zuhura ni jambo la kawaida miongoni mwa kaya za vijijini nchini Tanzania. Kwa upande wa Zuhura, ukosefu wa mapato ya kutosha, utambulisho sahihi na dhamana, pamoja na umbali wa vituo vya kutolea huduma za fedha hufanya iwe vigumu kwake kujihusisha na huduma hizi; wakati kwa upande wa watoa huduma, bado hawana bidhaa/huduma sahihi za fedha zinazoweza kukidhi mahitaji ya fedha ya Zuhura na kaya yake.
Hii inawaacha watu wengi wenye mahitaji kama ya Zuhura na kaya yake kutengwa au kuachwa nyuma katika kutumia na kunufaika na huduma rasmi za fedha.
Kwa hiyo, Vikundi vya Kijamii vya Huduma Ndogo za Fedha (CMGs) vilijitokeza kushughulikia changamoto na mapungufu hayo yaliyokuwepo katika sekta rasmi ya fedha. Kupitia Kikundi cha Kijamii cha Huduma Ndogo za Fedha cha Mapendano, Zuhura ameweza kuwapeleka watoto wake shule, kuipatia mahitaji ya msingi familia yake, kuanzisha shamba la kuku na kuwasaidia wengine katika jamii yake.
Hata hivyo, kwa kadri kikundi cha Mapendano kilivyoweza kukidhi mahitaji ya Uhura, kikundi kimepitia changamoto kadhaa kwa miaka mingi, ikiwa ni pamoja na kubadilisha Waweka Hazina wengi kutokana na wizi kwani michango yao na akiba zao zilihifadhiwa katika nyumba za Waweka Hazina; lakini pia kukosa katiba imara ya kuongoza shughuli zao kuliliacha kundi hicho kuwa katika hatari kubwa ya kuwakopesha wanakikundi wabaya/wasiolipa mikopo yao.
Mapema mwaka 2020, Kikundi cha Mapendano kilisikia kupitia ofisi yao ya Serikali za Mitaa kwamba kulikuwa na sheria mpya ambayo iliwataka kusajili kikundi chao. Matokeo yake, Zuhura na kikundi chake walianza kubashiri juu ya madhumuni ya sheria hiyo mpya na ikiwa ina manufaa kwa kikundi (CMG) chao. Miongoni mwa hofu ilikuwa ni kwamba sheria ilikuwa ni mbinu nyingine Serikali kukusanya kodi kutoka kwenye vikundi (CMGs).
Mapungufu ya ufahamu kwa umma juu ya dhamira ya sheria hiyo, yaliacha mianya kwa umma kuendelea kubashiri na kuendeleza wasiwasi dhidi ya sheria hiyo. Ubashiri na hofu iliyotokana na uwepo wa sheria hiyo ingeweza kuwa na athari hasi juu ya mapokezi ya Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya 2018 na Kanuni zake.
Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2017 (NMP 2017) na Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 ziliundwa, kwa lengo la kuwalinda watoa huduma na watumiaji wa huduma rasmi na zisizo rasmi za fedha nchini Tanzania.
Sheria hii inalenga kuongeza imani kwa umma katika sekta ya fedha kwa kutambua kuwa huduma ndogo za fedha ni huduma kuu za msingi zinazotumiwa na Watanzania walio wengi, hususani wa vijijini na wenye kipato cha chini, kama Zuhura. Sheria hii ni tosherevu kwa kuwa inagusia sekta nzima ya huduma ndogo za fedha kama inavyotambua madaraja tofauti ya watoa huduma ndogo za fedha (yaani Benki za Biashara / Jamii / Huduma ndogo za fedha, Taasisi za Huduma ndogo za fedha na Wakopeshaji binafsi wa fedha, Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo (SACCOS), pamoja na Vikundi Vya Kijamii Vya Huduma Ndogo za Fedha (CMGs) na inanda ufafanuzi wa kisera utakaofanya kazi kwa madaraja tofauti.
Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 itabadilisha mazingira kwa watoa huduma za fedha kwa kaya za vijijini na kuna uwezekano ikawezesha ongezeko la kuibuka kwa bidhaa, huduma, na majawabu yenye ufanisi katika kupunguza umaskini au kutoa mwongoz wa kujinasua kutoka lindi la umaskini.
Kufuata Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018 kuna manufaa makubwa kwa Vikundi vya Kijamii vya Huduma Ndogo za Fedha kutokana na sababu za msingi ikiwa ni pamoja na; kikundi kutambuliwa kisheria kama taasisi huru inayoweza kumiliki au kuuza mali, kuwa na ulinzi kisheria linapotokea tatizo, kuboresha uhusiano na watoa huduma rasmi za fedha ili wanakikundi waweze kunufaika na huduma mbalimbali za fedha za gharama nafuu, kuongeza usalama wa fedha zinazochangwa na wanachama endapo vikundi vitahifadhi michango ya wanachama kwenye akaunti benki; na vikundi vilivyosajiliwa vitafaidika na miradi mbalimbali ya Serikali inayolenga kuimarisha vikundi (CMGs).
Miongoni mwa faida muhimu za Sheria hii kwa CMGs ni kwamba sasa taarifa za wanachama wao na historia ya mikopo(yaani michango, ulipaji wa mikopo, chaguo-msingi juu ya ulipaji) itapatikana kwenye mifumo ya ubadirishanaji taarifa za wakopaji. Hii itasaidia katika kuwajulisha wana Kikundi juu ya wanachama uaminifu wanaofaa kujiunga na vikundi na kupewa huduma.
Kuhusu muundo na mpangilio, Sheria na kanuni za Huduma Ndogo za Fedha zinaeleza kuwa Kikundi cha Kijamii cha Huduma Ndogo za Fedha kinaweza kuundwa na watu 10 hadi 50, ambao wana dhana / lengo la pamoja. Wanachama wanapaswa kukutana ili kukubaliana juu ya uundaji wa kikundi, kujiwekea malengo,kuunda katiba, na kamati ambayo itawezesha uanzishwaji wa kikundi
Kanuni hizo pia zinavitaka Vikundi vya Kijamii Vya Huduma Ndogo kuwasilisha maombi ya usajili kwa Mamlaka husika ya Serikali za Mitaa kwa fomu maalumu ambayo itatolewa. Ofisi ya Rais Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa (OR -TAMISEMI) imekasimishwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kusimamia Vikundi nchini Tanzania.
Maombi yataambatana na nyaraka zifuatazo: nakala mbili za katiba zilizosainiwa na wanachama wote; nakala moja ya taarifa za mkutano wa kwanza wa uundaji wa kikundi uilosainiwa na washiriki wote wa mkutano wa awali; maazimio ya wanachama kuunda na kusajili kikundi cha kijamii; muundo wa kikundi uliopendekezwa na majina ya viongozi waliopendekezwa na kuidhinishwa na wanachama katika mkutano wa uundaji wa kikundi; orodha ya wanachama, ikiwa idadi ya wanachama ni kumi hadi hamsini kulingana na kanuni; ushahidi wa michango ya wanachama wa kikundi cha awali iliyowekwa katika Akaunti ya kikundi; barua ya utambulisho kutoka ofisi ya serikali ya kata au kijij au mtaa kuanzisha kikundi; na nyaraka au taarifa nyingine zozote zinazofaa.
Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha inatarajiwa kuimarisha Vikundi vya Kijamii (CMGs). Kabla ya utekelezaji wa sheria hii, sekta ndogo ya fedha ilikuwa inafanya kazi bila kudhibitiwa/kusimamiwa, na kuacha mianya uhalifu mwingi, upotevu, na udanganyifu mkubwa baina ya washiriki wa sekta hii ya huduma ndogo za fedha.
Kupitia Sheria hii, watumiaji wa huduma ndogo za fedha watalindwa na sheria dhidi ya wahalifu wowote, na kuleta muundo na mpaangilio bora ndani ya sekta ndogo ya Huduma Ndogo za Fedha. Hii itafungua njia ya kufanya Vikundi Vya Kijamii vya Huduma Ndogo za Fedha (CMGs) kuwa endelevu na kuwezesha huduma hizi kuwa na thamani zaidi kwa wanachama.