Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amezindua studio za kidijiti za redio ikiwa ni sehemu ya mradi wa maboresho ya studio za redio, televisheni na mitandao ya kijamii za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Amezindua studio hizo za kisasa leo (Jumamosi, Aprili 20, 2024) kwenye hafla iliyofanyika kwenye studio za shirika hilo, barabara ya Nyerere, jijini Dar es Salaam.
“Nimefurahi sana baada ya kujulishwa kuwa uzinduzi wa mradi huu umezingatia awamu ya tatu ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026). Mpango huo umeainisha vipaumbele katika uwekezaji wa miundombinu ya utangazaji ya TBC, ikiwemo upanuzi wa usikivu wa redio, ununuzi wa mitambo na vifaa vya redio na televisheni.”
Akiwa kwenye studio hizo, Waziri Mkuu alikagua studio za kisasa na kufanyiwa mahojiano mafupi kwenye studio ya TBC Taifa ambako alieleza jinsi alivyofanyiwa usaili wa kazi ya utangazaji mwaka 1994.
Waziri Mkuu amesema alifanikiwa kupata kazi hiyo lakini kabla hajaripoti akawa amechaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. “Nilitakiwa kuanza kazi Julai 10, 1994 lakini matokeo ya kwenda Chuo Kikuu yakatoka mwezi Juni. Wazee wakanishauri nikasome kwanza, nikimaliza nitakuja kuomba kazi, lakini baada ya chuo, nikaishia hukooo.”
Pia alitembelea studio za TBC International na Bongo FM ambako alikuta vijana ndiyo wanashika usukani wa kuendesha mitambo na vipindi na kuelezwa na Mkurugenzi wa Huduma za Redio, Bi. Aisha Dachi kwamba maudhui yake yamewalenga zaidi vijana.
Naye, Waziri ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema mafanikio hayo yote yanatokana na utashi wa kisiasa wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuamua kuwekeza kwenye shirika hilo.
Kwa upande wake, Waziri Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wa SMZ, Tabia Maulid Mwita alimshukuru Waziri wa Habari, Nape Nnauye kwa kuwasaidia Tume ya Utangazaji Zanzibar kupitia TCRA kwa kuwapatia vifaa vya sh. milioni 45.
Mapema, Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dkt. Ayub Rioba alimweleza Waziri Mkuu kwamba shirika hilo hivi sasa ni miongoni mwa vyombo vya habari vya kupigiwa mfano barani Afrika.
Aliishukuru Serikali kwa kutoa fedha nyingi ambazo zimesaidia kukamilisha maboresho yaliyokuwa yakifanyika. “Matengenezo yote yamegharimu shilingi bilioni 5.7, tunaishukuru Serikali kwa kuleta fedha hizi. Tanzania imepiga hatua sana kwenye utangazaji, tunamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha hizi,” alisema.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Suleiman Kakoso aliitaka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii ziwe zinaitumia TBC kuandaa vipindi vipya ambavyo vitatumika kuitangaza nchi.
Kuhusu upatikanaji wa vifaa kwa shirika hilo, Kakoso alisema: “Ili iweze kufanya kazi kwa ufanisI, TBC inahitaji kupatiwa magari manane ya kurushia matangazo kwenye kanda zake zote ambayo yatagharimu shilingi bilioni 20.”
Wakati huohuo, Waziri Mkuuamewataka wananchi wote wawe wazalendo na mabalozi wazuri wa kutangaza kazi nzuri zilizofanywa na Serikali ya awamu ya sita.
“Watanzania wote kupitia hadhara hii, tushikamane tumuunge mkono Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuleta maendeleo, kuinua ustawi wa wananchi na kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchumi na maendeleo,” amesema.
Ametoa wito huo wakati akifunga tamasha la “MITATU YA KISHINDO, KAZI INAONGEA” lililoandaliwa na Uhuru Media Group (UMG) katika viwanja vya TTCL, Kijitonyama, Dar es Salaam.
Amesema katika dunia ya leo, kila Taifa lina utamaduni wake na utashi wake, na kila Taifa linahamasisha wananchi wake kulinda kilicho chake kwa maslahi ya kizazi kilichopo na vizazi vijavyo. “Natoa rai kwa vyombo vya habari, kujenga utamaduni wa kuchapisha maudhui na habari zenye athari chanya kwa Taifa letu.”
Amewasihi wananchi wajitokeze kutoa maoni ya kuchangia Dira mpya ya Taifa ya Maendeleo. “Hii ni haki ya kila mwananchi kutoa maoni yatakayotumika kutoa mwelekeo na kupanga mipango ya maendeleo ya Taifa letu,” amesisitiza.