Kumekuwa na maswali mengi ya kutaka kujua kuhusu Roboti Eunice aliyekuwa Bungeni siku ya uwasilishwaji wa Bajeti ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Roboti Eunice aliletwa Bungeni kuonesha (kushowcase) bunifu za Africa kwenye (Akili Mnemba (AI) and Robotics. Tanzania ni mwenyeji wa kilele cha shindano la Afrika-AU kwenye masuala ya robotics na Akili Mnemba (Artificial Intelligence).
Mashindano haya yanaendeshwa na kusimamiwa na Umoja wa Africa (AU NEPAD) na ELevate AI ambalo ni Shirika la Kimataifa na mwanzishaji wake ni Mtanzania).
Roboti Eunice yupo nchini kuhamasisha vijana wa Kitanzania kushiriki shindano hilo kuelekea shindano hilo. Nia ni kuwahamasisha vijana wetu wajitokeze kwa wingi kushiriki shindano hilo na kuiweka Tanzania kwenye ramani ya masuala ya Akili Mnemba na Robotiki ambalo ni moja ya vipaumbele vya Bajeti ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa Mwaka 2024/25.
Kuna baadhi ya watu wamekuwa wakimbeza kwa kumfananisha Roboti Eunice na Roboti za hali ya juu (advanced models) za Roboti waliotengenezwa na nchi zilizoendelea kama vile China, Marekani na Urusi ambao walianza siku nyingi kutengeneza Roboti.
Hata hivyo ikumbukwe lengo la Serikali kupitia Wizara yenye dhamana ya TEHAMA ni kuleta chachu kwa Vijana wa Kitanzania kuwa upo uhitaji wa Vijana wa Tanzania kuunda Roboti walioundwa kwa viwango vya hali ya juu na kuzungumza lugha zetu kuendana na changamoto za mazingira ya Kitanzania.
Tuwaunge mkono vijana wetu badala ya kuwakebehi ili wasiogope hata kujaribu “kutembea kabla ya kukimbia”. Tukumbuke msemo usemao “hata mbuyu ulianza kama mchicha.
Shime vijana wa Tanzania tuwe sehemu ya mabadiliko na kushiriki ubunifu wa akili Mnemba na Roboti na tusiogope changamoto na kebehi.