Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza taarifa maalum ya udhibiti wa vitendo vya uvuvi haramu iwasilishwe kabla ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi haijawasilisha hotuba ya bajeti ya mwaka 2024/2025.
Ametoa agizo hilo leo katika hafla ya uzinduzi wa boti maalum kwa ajili ya kukabiliana na vitendo vya kihalifu katika bahari hapa nchini iliyofanyika bandarini jijini Dar es Salaam.
“Taarifa kuhusiana na shughuli maalum ya udhibiti wa vitendo vya uvuvi haramu katika ukanda wa Bahari kuu iwasilishwe kabla ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi haijawasilisha hotuba ya bajeti ya mwaka 2024/2025,” amesema.
Ameishukuru Serikali ya Japan kwa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kufanikisha mipango ya maendeleo ambayo imechangia dola za Marekani 500,000 kwenye ununuzi wa boti hiyo. “Ninaiomba Serikali ya Japan isichoke kutusaidia ili tuweze kukamilisha utekelezaji wa mikakati iliyopo katika eneo hili la kukabiliana na uhalifu nchini,” amesema.
Vilevile, amelishukuru Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa kuchangia dola za Marekani 400,000 kwenye mradi huo. “Mchango wenu tunauthamini sana, wakati wote mmekuwa mkishirikiana nasi katika maeneo mengi, kwa niaba ya wananchi na Serikali ya Tanzania ninawashukuru sana,” amesema.
Mapema, akitoa taarifa ya mradi huo mbele ya Waziri Mkuu, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Ummy Nderiananga alieleza kuwa ununuzi wa boti hiyo ni sehemu ya mafanikio ya utekelezaji wa Mradi wa Kukabiliana na Vitendo vya Kihalifu katika Bahari na Maziwa Makuu unaotekelezwa na Serikali.
Alisema mapambano hayo yatahusisha kuimarisha juhudi za kukabiliana na vitendo vya kihalifu kama vile uvuvi haramu, uhamiaji haramu, uharamia, usafirishaji wa dawa za kulevya na utoroshwaji wa nyara za Serikali.
Akieleza sifa za boti hiyo alisema: “Ni boti ni mpya, ya kisasa yenye uwezo mkubwa wa kuhimili utekelezaji wa majukumu ya doria. Boti hii ya doria imepewa jina la Patrol Boat Sailfish (PB Sailfish).”
Amesema uwepo wa boti hiyo utaleta mageuzi makubwa kwenye ulinzi na usalama wa baharini kwani itawezesha kufanya doria na kaguzi kwenye maji ya Tanzania. “Itafanya utafutaji na uokozi pindi zikitokea ajali baharini na kuimarisha ulinzi kwenye pwani yetu kwa kuwa imewekewa mitambo maalum ya silaha pamoja na mtambo maalum wa kuzima moto… boti hii ni mwarobaini wa kuhakikisha pwani ya Tanzania iko salama.”
Kwa upande wake, Balozi wa Japan nchini, Yasushi Misawa amesema nchi yake itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika mapambano hayo na kueleza umuhimu wa mradi kuwa utaimarisha uwezo wa Tanzania wa kuzuia shughuli haramu ndani ya bahari ya Tanzania.
Alitumia fursa hiyo kueleza kuwa nchi yake itaendelea kuimarisha mahusiano wa kirafiki uliopo baina ya nchi hizo mbili kwa zaidi ya miaka 60 tangu uhuru wa Tanzania. “Kwa mtazamo wa usafiri wa majini, JICA imeamua kutoa fedha zaidi kwa ajili ya mradi wa ukaratbati wa bandari ya Kigoma. Japan pia kwa muda mrefu imekuwa ikiisaidia Tanzania katika kukuza sekta ya uvuvi,” alisema Balozi Misawa.
Naye, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega ameishukuru Serikali kwa kupatikana kwa boti ya doria kwenye bahari na maziwa makuu kwa sababu itatatua changamoto ya uhalifu.
Ameishukuru Serikali kwa kupambana na milipuko baharini pamoja na kuwakabili wahusika wa vilipuzi ambapo hadi sasa watuhumiwa wapatao 24 wamekwishakamatwa. “Kati ya hao, 13 ni wasambazaji wa vilipuzi, 10 ni wavuvi na mmoja ni mfadhili wao,” alisema.
Amesema jitihada zinazafanyika kudhibiti vitendo hivyo katika maeneo yote ya ukanda wa bahari ya Hindi na baadaye nguvu zitaelekezwa kwenye maziwa makuu.
Akitoa taarifa kuhusu ufanisi boti hiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Brigedia Jenerali Hosea Ndagala alisema boti hiyo ina uwezo kukimbia kwa kasi ya km. 47 kwa saa (nautical miles 25), inaweza kubeba wahalifu 20 kwa pamoja, inaweza kutumika kubebea wagonjwa (ambulance), kuzima moto na kwenye shughuli za uokoaji.