Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mhe. Sixtus Mapunda ameitaka timu ya wataalamu wa mazingira na ustawi wa jamii ya TARURA na wilaya ya Temeke kukaa pamoja na kutengeneza mpango kazi mzuri wa uwasilishwaji wa taarifa za utunzaji wa mazingira katika wilaya yake.
Mhe. Mapunda ameyasema hayo katika kikao cha pamoja baina yake na timu ya TARURA kilichofanyika katika ofisi yake ikiwa ni muendelezo wa kampeni ya kutekeleza sheria za kutunza na kulinda mazingira kwenye mitaro ya Barabara kwa kushirikiana na wilaya zilizopo mkoa wa Dar es Salaam.
Mhe. Mapunda ameipongeza TARURA kwa kazi nzuri wanazofanya katika sekta ya miundombinu ya barabara wilayani Temeke na ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa kutosha katika ulinzi wa Miundombinu hiyo.
Timu ya wataalamu kutoka TARURA ikiongozwa na Meneja wa TARURA mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi Geofrey Mkinga na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mazingira na Ustawi wa Jamii Bi. Leticia Mapunda inaendelea kufanya mazungumzo na Wakuu wa Wilaya kwa lengo la kufanya uhamasishaji kuhusu usimamizi wa sheria ya mazingira zilizo chini ya mamlaka ya Manispaa na Jiji katika Mkoa wa Dar es Salaam.