Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania-TFS umeshiriki na kufadhili mkutano wa kitaaluma wa Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini uliolenga kuhamasisha uandishi wa habari katika matumizi ya gesi ili kulinda misitu.
Akifungua mkutano huo Jijini Dodoma mapema hivi leo Aprili 29, 2024, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema Serikali itahakikisha matumizi ya gesi yanapewa kipaumbele na kufanya jitihada ili kupunguza gharama za mitungi ya gesi.
“Ifikapo mwaka 2034 tunataka asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia” Dkt. Biteko.
Nae Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Meneja Sehemu ya Baiolojia Mbegu za Miti Fandey Mashimba, akitoa wasilisho kuhusu kazi za TFS, ameomba ushirikiano wa wahariri katika kufikisha elimu kwa umma na namna ya kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya misitu na nyuki.
TFS ilipewa Cheti cha ufadhili kilichopokelewa na Meneja Uhusiano, Johary Kachwamba kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi-TFS, Prof. Dos Santos Silayo.