Hotuba ya bajeti ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf f. Mkenda aliowasilisha Bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2024/2025,inaaonyesha Bajeti ni ya jumla ya bajeti ni shilingi 1,97 trillion.
Vipaumbele hivi:
Katika mwaka wa fedha 2024/25, Wizara imepanga kutekeleza vipaumbele vitano vyenye lengo la kuongeza ubora wa elimu kwa kuwezesha vijana wa Kitanzania kupata maarifa, ujuzi, kujiamini, kujiajiri na kuajirika. Vilevile, vipaumbele vyenye kujielekeza katika kutegemeza tafiti, sayansi, teknolojia na ubunifu katika agenda ya maendeleo ya nchi.
Vipaumbele vya Wizara kwa mwaka wa fedha 2024/25 ni kama vifuatavyo:
- kuendelea na utekelezaji wa sera na mitaala, mapitio ya sheria na kuandaa miongozo ya utoaji elimu na mafunzo nchini;
- kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi (amali na amali sanifu);
- kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya msingi, sekondari na ualimu;
- kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya juu; na
- kuendeleza tafiti, matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu.
- Kuendelea na utekelezaji wa Sera na Mitaala, Mapitio ya Sheria na kuandaa Miongozo ya Utoaji Elimu na Mafunzo Nchini
Serikali itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Toleo la 2023 na Mitaala kwa ngazi ya Elimu ya Msingi, Sekondari na Ualimu. Aidha, itaendelea na uandaaji wa zana za utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Toleo la 2023 ambazo ni Miongozo, Mfumo wa Kitaifa wa Tuzo na Sifa Linganifu (Tanzania Qualification Framework – TQF), Sheria na Kanuni, Mfumo wa Mtaala wa Kitaifa na Mfumo wa Tathmini wa Kitaifa katika ngazi ya Elimu ya Msingi, Sekondari, Ualimu, Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi na Elimu ya Juu kwa lengo la kuwezesha ufanisi katika utekelezaji wa Sera.
Serikali itaendelea na maboresho ya mitaala ya elimu ya amali sanifu na elimu ya juu ili kuwezesha nchi kuandaa rasilimaliwatu yenye ujuzi na maarifa. Katika kufikia azma hiyo, Serikali itatekeleza yafuatayo:
- itafanya mapitio ya mitaala 171, kuandaa mitaala mipya 18, kuanzisha programu za vipaumbele 145 pamoja na matumizi ya mbinu bunifu za ufundishaji katika elimu ya juu. Aidha, itawezesha ziara za kimkakati kwa wafanyakazi wa sekta ya elimu katika nchi zenye uzoefu wa uandaaji wa rasilimaliwatu yenye maarifa na ujuzi wenye kuchangia katika ukuaji wa kati wa uchumi;
- itasasisha na kuandaa mtaala mpya katika taasisi 17 za elimu ya juu; na
- itahakiki mitaala 230 ya vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi. Lengo ni kuhakikisha kuwa mafunzo yanayotolewa yanakidhi mipango ya nchi, soko la ajira la kitaifa na kimataifa na kuwawezesha wahitimu kujiajiri na kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira.
Serikali itaendelea kutoa elimu kuhusu maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Toleo la 2023 kwa watendaji wa ngazi zote za elimu na mafunzo wakiwemo walimu wa shule za msingi; walimu wa shule za sekondari; wakufunzi wa vyuo vya ualimu; wakufunzi wa vyuo vya ufundi; wakufunzi wa vyuo vya VETA; wakufunzi wa vyuo vya maendeleo ya wananchi; maafisa elimu msingi, maafisa elimu sekondari, wasimamizi wa elimu ngazi ya mkoa; maafisa elimu kata; wathibiti ubora wa shule; na wanataaluma kutoka taasisi za elimu ya juu. Vilevile,itaendelea kutoa mafunzo kazini kwa walimu wa shule za msingi na sekondari kuhusu mitaala iliyoboreshwa.
Serikali itaendelea na mapitio ya Sheria ya Elimu, Sura 353 ili iendane na Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Toleo la 2023. Vilevile, itafanya mapitio ya sharia na miundo ya taasisi mbalimbali ikiwamo; COSTECH, TLSB, NECTA, VETA, TCU, NACTVET, TIE, TEWW na TEA ili ziendane na maboresho ya Sera na Sheria na makuliano mbalimbali ya Kikanda na Kimataifa. Vilevile, itafanya marekebisho ya Sheria ya Bodi ya Mikopo kwa lengo la kuongeza ufasini wake ikiwamo kurahisisha ufunguaji wa mashauri na utekelezaji wake.
Serikali itaendelea kuhuisha miongozo mbalimbali ya utoaji elimu na mafunzo nchini ili kuendana na maboresho ya Mitaala na Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Toleo la 2023 kama ifuatavyo:
- itakamilisha Mwongozo wa Kuwatambua na Kuwaendeleza Wanafunzi wenye Vipawa na Vipaji; na
- itaandaa Mwongozo wa Elimu Jumuishi wa Ufundishaji na Matumizi ya Teknolojia kwa lengo la kuongeza ufanisi katika ufundishaji na matumizi ya teknolojia katika elimu na mafunzo.
Serikali itaongeza wigo wa ukusanyaji, uchakataji na utoaji wa takwimu za elimu kwa kuunganisha mifumo yote ya takwimu za elimu ya awali, msingi, sekondari, ualimu, ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, elimu ya juu, pamoja na mifumo ya upimaji na tathmini. Maboresho hayo yatahusisha kujumuisha taarifa za shule binafsi zisizo tumia mitaala ya Taifa. Mabadiliko hayo yatawezesha Wizara kuwa na taarifa za kila mwanafunzi, fani na programu zinazotolewa nchini na kuandaa Kitabu cha Taifa cha Takwimu Muhimu za Elimu (Basic Education Statistics in Tanzania – BEST) ambacho kitakuwa na taarifa za kuanzia elimu ya awali hadi elimu ya juu. Kazi ya maboresha hayo imeshaanza na inafanywa na wataalamu wa ndani kutoka vyuo vikuu. Aidha, Serikali itaanzisha jukwaa shirikishi la utafiti la wadau wa elimu ambalo litatambua na kuratibu tafiti za kielimu zinazofanyika nchini. Lengo ni kuhakikisha kuwa maamuzi ya kimageuzi na maendeleo katika sekta yanazingatia taarifa, takwimu na tafiti sahihi zenye maslahi kwa sekta na Taifa kwa ujumla.
Katika kuhakikisha tunaimarisha matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu katika agenda ya maendeleo, Serikali itaendelea na mapitio ya Sera ya Sayansi na Teknolojia ya Mwaka 1996 kwa lengo la kuandaa sera inayoakisi hali ya sasa na ya baadaye ya maendeleo ya sayansi, teknolojia na ubunifu.
Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya vyuo vya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi pamoja na sekondari za amali ili kuongeza fursa za mafunzo kwa kutekeleza yafuatayo:
- itawezesha ujenzi wa shule mpya za sekondari za amali za uhandisi 100 kati ya hizo shule 26 zitaanza kupokea wanafunzi kuanzia Januari 2025. Aidha, ujenzi wa shule za amali utapewa kipaumbele katika maeneo ambayo hayana vyuo ya mafunzo ya ufundi stadi;
- itaendelea na ujenzi wa vyuo 65 vya mafunzo ya ufundi stadi, kati ya hivyo 64 ni vya wilaya na kimoja ni cha ngazi ya Mkoa wa Songwe. Vilevile, imeongeza vifaa vya kufundishia na kujifunzia katika vyuo 29 vilivyokamilisha ujenzi;
- itaendelea na ujenzi wa miundombinu ya nyongeza katika vyuo 10 vya mafunzo ya ufundi stadi (Ndolage-Muleba, Ileje, Newala, Ngorongoro, Gorowa – Babati, Urambo, Kasulu, Mabalanga – Kilindi, Nkasi na Kanadi – Bariadi) ili kuviwezesha vyuo hivyo kufikia viwango vya msingi vya utoaji wa mafunzo; na
- itaendelea na ujenzi wa hosteli mbili katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere – Kampasi ya Karume zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 768 kwa kila hosteli. Vilevile, itaendelea na ujenzi wa maktaba yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 2,500, ukumbi wa mihadhara utakaohudumia wanafunzi 1,000 kwa wakati mmoja na itajenga madarasa 12 yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 300 kwa kila darasa na ofisi 20 za watumishi katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere – Kampasi ya Kivukoni. Aidha, itaendelea na ujenzi wa jengo la utawala na madarasa yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 1,800 katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere – Kampasi ya Pemba. Aidha, itaendelea na ujenzi wa miundombinu mbalimbali katika vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.
Serikali itaendelea kuongeza fursa za mafunzo ya amali (elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi) katika vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi. Katika kufikia azma hiyo, Serikali itatekeleza yafuatayo:
- itasajili vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi 150 ambapo vyuo vya elimu ya ufundi ni 100 na vyuo vyamafunzo ya ufundi stadi ni 50,hivyo kuwa na jumla ya vyuo 504 vya elimu ya ufundi na vyuo 885 vya mafunzo ya ufundi stadi. Usajili wa taasisi hizo utawezesha kuongeza fursa na kutoa mafunzo kwa kuzingatia viwango na ubora;
- itadahili wanafunzi 263,718 wa elimu ya ufundi na mafunzo na ufundi stadi ambapo wanafunzi wa vyuo vya elimu ya ufundi ni 190,518 na wanafunzi wa vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi ni 73,200 sawa na ongezeko la asilimia 23 ikilinganishwa na udahili wa mwaka 2023/24. Udahili unalenga kuongeza rasilimaliwatu yenye ujuzi na uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa;
- itatoa mikopo kwa wanafunzi wa stashahada takribani 10,000 katika fani za kipumbele na zenye uhaba wa wataalam nchini ikiwamo fani sayansi na ufundi; na
- itadahili wanafunzi 2,089 katika Chuo cha Ualimu wa Mafunzo ya Ufundi Stadi Morogoro – MVTTC ili kuongeza idadi ya walimu wanaofundisha vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi na vyuo vya ualimu wa mafunzo ya ufundi.
- Katika kuwajengea umahiri walimu wa vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi pamoja na vyuo vya maendeleo ya wananchi, Serikali itatekeleza yafuatayo:
- itatoa mafunzo kwa walimu 1,000 wa vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi kuhusu tathmini ya mitaala ya umahiri ili kuwawezesha walimu kufundisha na kufanya tathmini ya wanafunzi kwa kuzingatia umahiri; na
- kuendelea kuboresha vituo vya umahiri kwa ajili ya kuimarisha utoaji wa mafunzo wa fani za kipaumbele kupitia Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam, Chuo cha Ufundi Arusha na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji.
Katika kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika ngazi ya elimu ya msingi, sekondari na ualimu, Serikali itatekeleza yafuatayo:
- itawezesha ujenzi wa shule za sekondari za kata 226, nyumba za walimu 184 wa sekondari na ununuzi wa vifaa vya maabara;
- itawezesha ujenzi wa madarasa 2,018 (msingi 1,221 na sekondari 797); mabweni 114 kwa shule za sekondari; nyumba za walimu 658 (msingi 567 na sekondari 81) matundu ya vyoo 2,848 (msingi 1,514 na sekondari 884), maabara 10 na vituo vya walimu (TRCs) 300 kwa lengo la kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji. Aidha, itakamilisha ujenzi vyumba vya madarasa 111 katika shule za msingi 37, matundu ya vyoo, maabara, nyumba za walimu na mabweni katika shule za sekondari 50; na
- itaweka nishati safi ya kupikia ili kuendelea kuhifadhi na kuimarisha mazingira katika vyuo vya ualimu 11 (Nachingwea, Katoke, Kleruu, Tabora, Dakawa, Patandi, Mpwapwa, Sumbawanga, Mhonda, Kasulu na Monduli). Vilevile, itanunua samani kwa ajili ya Chuo cha Ualimu Sumbawanga, Mhonda, Dakawa na Ngorongoro.
Serikali itaendelea kutoa ithibati kwa shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu kwa kutekeleza yafuatayo:
- itasajili shule za msingi na sekondari takribani 772 ambapo awali pekee 30, awali na msingi 475 (zisizo za Serikali 162), sekondari 266 (zisizo za Serikali 57), chuo cha ualimu kimoja cha binafsi; na
- itafanya tathmini kwa shule 100 zilizopewa usajili wa masharti ili kubaini utekelezaji wa masharti ya usajili.
Katika kuimarisha uthibiti ubora wa shule za msingi, sekondari, vyuo vya ualimu na vyuo vya maendeleo ya wananchi, Serikali itatekeleza yafuatayo:
- itafanya tathmini ya jumla katika asasi 6,620 (shule za awali na msingi 4,965, sekondari 1,525, vyuo vya ualimu 66, vyuo vya maendeleo ya wananchi 14, na vituo 50 vya elimu ya watu wazima na mafunzo nje ya mfumo rasmi). Vilevile, itafanya ufuatiliaji na tathmini kwa lengo la kubaini ubora katika uandikishaji, ufundishaji na ujifunzaji, usimamizi na uongozi na kutoa ushauri kwa walimu wa masomo katika taasisi 1,010;
- itaendelea na ujenzi wa ofisi ya uthibiti ubora wa shule katika Halmashauri ya Wilaya ya Mlele na ukarabati wa ofisi nne za uthibiti ubora wa shule katika Halmashauri ya Mpwapwa, Chato, Mpanda, na Halmashauri ya Mji – Ifakara;na
- itanunua samani na vitendea kazi katika ofisi 210 (halmashauri 184 na mikoa 26) za uthibiti ubora wa shule na itanunua magari 3 kwa ajili ya shughuli za uthibiti ubora wa shule katika Halmashauri ya Mlele, Tunduma na Serengeti.
Serikali itaendelea kuimarisha upatikanaji wa vitabu katika ngazi ya elimu ya awali, msingi na sekondari kwa lengo la kuimarisha uwiano wa kitabu kwa mwanafunzi na hivyo kuboresha ufundishaji na ujifunzaji na kuchochea tabia na utamaduni wa kujisomea kwa kutekeleza yafuatayo:
- itachapa na kusambaza nakala za vitabu 2,000,000 vya masomo ya Hisabati na Sayansi kwa kidato cha 1 hadi 4;
- itaandaa vitabu vya kiada kwa darasa la II na IV, sekondari kidato cha 1 na cha 6 na viongozi vya mwalimu. aidha, itaweka maudhui ya elimu ya sekondari katika mfumo wa kidijiti kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wake;
- itachapa na kusambaza vitabu vya kiada kwa darasa la ii na iv, sekondari kidato cha 1 na cha 6 na viongozi vya mwalimu; na
- itachapa na kusambaza vitabu vya kiada katika maandishi yaliyokuzwa na breli kwa darasa la II na IV, sekondari kidato cha 1 na cha 6 na viongozi vya mwalimu kwa ajili ya wanafunzi wenye uoni hafifu na wasioona kwa lengo la kuboresha ufundishaji na ujifunzaji kwa watoto wenyemahitaji maalum.
Serikali itaendelea kukuza ujuzi wa uandishi na kuhamasisha tabia ya usomaji na kuimarisha matumizi ya maktaba katika ngazi zote za elimu kwa kutekeleza yafuatayo: ilevile, Serikali itaendelea kukuza ujuzi wa uandishi na kuhamasisha tabia ya usomaji na kuimarisha matumizi ya maktaba kwa kutekeleza yafuatayo:
- itaandaa Rasimu ya Sera ya Taifa ya Huduma za Maktaba nchini. Vilevile, itaendelea kununua vitabu kwa ajili ya maktaba za mkoa na kuendeleza Maktaba 15 za Jamii;
- itaendelea kusimamia na kuratibu utoaji wa Tuzo ya Kitaifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu yenye lengo la kuhamasisha uandishi na usomaji wa vitabu, kutunza historia na utamaduni wa Mtanzania na kuinua sekta ya uchapaji nchini. Tuzo hizo zitatolewa kwa waandishi mahiri wa riwaya, hadithi fupi na ushairi;
- itagharamia uchapaji, kununua na kusambaza katika taasisi za elimu na maktaba vitabu vya washindi wa tuzo hizo. Mafanikio katika azma hii yamelenga kuwezesha sekta ya uchapishaji na uchapaji na kuongeza ari ya kusoma; na
- itaendelea kuratibu na kukuza stadi na ujuzi wa uandishi insha kwa wanafunzi wa elimu ya msingi, sekondari na elimu ya juu nchini katika nyanja za: ujenzi wa taifa, mageuzi ya kimaendeleo, ustahimilivu na maridhiano. Tutaandaa shindano maalum la uandishi wa insha kwa wanafunzi kuchochea uelewa na fikra tunduizi kuhusu falsafa ya 4Rs ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vilevile, Serikali itaendelea kuratibu shindano la uandishi wa insha kwa Nchi za Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika kwa wanafunzi 2,000 wa shule za sekondari.
Serikali itanunua vifaa vya maabara kwa ajili ya shule za sekondari 1,322 na vyuo 13 vya ualimu pamoja na vifaa vya kufundishia na kujifunzia katika vyuo 35 vya ualimu. Vilevile, itanunua vifaa vya kujifunzia na kemikali kwa ajili ya kufundishia masomo ya sayansi kwa wanafunzi wa elimu kwa njia mbadala kwa hatua ya I na II.
Serikali itaimarisha utoaji wa elimu jumuishi kwa wanafunzi na walimu wenye mahitaji maalum kwa lengo la kuondoa vikwazo vya kimfumo na kimuundo ili kurahisisha ufundishaji na ujifunzaji kwa kutekeleza yafuatayo:
- itafanya tathmini ya awali ya kubaini hali ya usaidizi uliopo na unaohitajika kwa wanafunzi 1,000 na walimu 200 wenye mahitaji maalum kwa lengo la kutoa ushauri wa kitaalam;
- itajenga uelewa kwa jamii na wadau wa elimu kuhusu elimu jumuishi kwa lengo la kuhamasisha uandikishaji wa wanafunzi wenye mahitaji maalum;
- itawajengea uwezo maafisa 368 wa elimu maalum msingi na sekondari kuhusu ubainishaji wa awali wa watoto wenye ulemavu kwa lengo la kurahisisha zoezi la upimaji kwa kiwango kinachohitajika; na
- itanunua na kusambaza vifaa vya kufundishia na kujifunzia na vifaa saidizi kwa wakufunzi 105, walimu 103 na walimu tarajali 188 wenye mahitaji maalum ili kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji.
Serikali itaendelea kufanya upimaji na tathimini ya elimu ya msingi, sekondari na vyuo vya ualimu kwa kutekeleza yafuatayo:
- itaendesha Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne na Kidato cha Pili kwa watahiniwa 1,681,490 na 882,314 mtawalia wanaotarajiwa kufanya upimaji huo mwezi Novemba, 2024;
- itaendesha Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi kwa watahiniwa 1,241,291 wanaotarajiwa kufanya mtihani huo mwezi Septemba, 2024;
- itaendesha Mtihani wa Kidato cha Nne na Mtihani wa Maarifa kwa watahiniwa 559,646 wanaotarajiwa kufanya mitihani hiyo mwezi Novemba, 2024;
- itaendesha Mtihani wa Kidato cha Sita kwa watahiniwa 114,500 wanaotarajiwa kufanya mtihani huo mwezi Mei, 2025; na
- itaendesha Mtihani wa Cheti na Stashahada ya Ualimu kwa watahiniwa 8,500 wanaotarajiwa kufanya mtihani huo mwezi Mei, 2025.
- Kuongeza Fursa na Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Juu
Ili kuwezesha na kuimarisha huduma ya utoaji na upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu wenye sifa na uhitaji, Serikali itatekeleza yafuatayo:
- itaongeza fursa za mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kutoka 223,201 hadi 252,245;
- itatoa mikopo kwa wanafunzi 84,500 wa mwaka wa kwanza ambapo shahada ya kwanza 80,000, shahada za juu 2,000, wanaosoma nje ya nchi 500 na SAMIA Skolashipu 2,000. Aidha, itatoa mikopo kwa wanafunzi 157,745 wanaoendelea na masomo;
- itatoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 40 wenye ufaulu wa juu kwenye masomo ya sayansi hususan wanafunzi wa kike waliohitimu Mtihani wa Taifa ya Kidato cha Sita na shahada ya awali kupitia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam;
- itaendelea kukusanya madeni ya mikopo iliyoiva ya kiasi cha Shilingi Bilioni 198 kutoka sekta ya umma na kuimarisha makusanyo kutoka sekta binafsi na isiyo rasmi. Aidha, itatafuta wanufaika wapya 40,000 wenye marejesho ya mikopo iliyoiva ikijumuisha wanufaika wapya 5,000 wenye mikopo chechefu kutoka sekta binafsi na isiyo rasmi; na
- itaanza kutoa ufadhili kwa ajili ya shahada za juu ikiwemo eneo la fani ya mionzi na nyuklia.
Serikali itaendelea kutoa ithibati na uthibiti wa ubora wa elimu katika ngazi ya elimu ya juu kwa kutekeleza yafuatayo:
- itaendelea kuratibu udahili wa wanafunzi 145,800 wa mwaka wa kwanza wanaotarajiwa kujiunga na programu mbalimbali za masomo katika vyuo vya elimu ya juu; na
- itafanya tathmini ya maombi ya utambuzi wa tuzo 5,000 za wahitimu zilizotolewa katika vyuo vikuu vya nje na kuzitambua zitakazokidhi vigezo.
Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya taasisi za elimu ya juu ili kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa kutekeleza yafuatayo:
- itajenga miundombinu katika taasisi za elimu ya juu kupitia Mradi wa Kuendeleza Elimu ya Juu kwa ajili ya Mabadiliko ya Kiuchumi kama ifuatavyo: kumbi 27 za mihadhara; ofisi 302; vyumba 90 vya madarasa na vyumba 17 vya semina. miundombinu hiyo itajengwa katika kampasi 15 za vyuo vikuu katika mikoa ifuatayo: UDSM (Kagera, Lindi na Zanzibar); MUHAS (Kigoma); ARU (Sengerema-Mwanza); SUA (Katavi); Mzumbe (Tanga); MUST (Rukwa); UDOM (Njombe); MoCU – (Shinyanga); IAA (Manyara na Ruvuma); TIA (Singida); IFM (Simiyu). Vilevile, itaendelea na ujenzi wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius Nyerere cha Kilimo na Teknolojia Kampasi Kuu Butiama ambapo chuo hicho kitajenga kampasi yake mkoani Tabora; na
- itaendelea na ujenzi na ukarabati wa miundombinu mbalimbali katika taasisi za elimu ya juu ikiwemo ujenzi wa maabara, madarasa na hosteli.
Serikali itaendelea kuongeza idadi ya wanataaluma wenye sifa na kuwajengea uwezo watumishi wasio wanataaluma katika taasisi za elimu ya juu ambapo itagharamia mafunzo kwa wanataaluma 308 na watumishi wasio wanataaluma 23 kwa ngazi ya umahiri na shahada ya uzamivu katika fani mbalimbali.
Serikali itaweka mazingira wezeshi kwa kuboresha mifumo ya TEHAMA inayounganisha taasisi za maendeleo ya tafiti, taasisi za elimu ya juu na mifumo ya uratibu wa utafiti na ubunifu ili kurahisisha utendaji wa kazi na upatikanaji wa takwimu mbalimbali zinazohusu utafiti, ubunifu na maendeleo. Vilevile, itaunganisha mifumo ya takwimu za elimu na mafunzo nchini kuanzia ngazi ya elimu ya awali hadi elimu ya juu ili kuimarisha utoaji wa taarifa za elimu na mafunzo.
Serikali itaendelea kuimarisha taasisi za elimu ya juu na taasisi za kitafiti kuendelea kufanya utafiti wa kimkakati na kuongeza mchango wake katika ajenda ya maendeleo ya Taifa na kuboresha ustawi wa jamii kwa kutekeleza yafuatayo:
- itaandaa mikakati ya utekelezaji na usambazaji wa matokeo ya utafiti;
- itafanya tafiti 301 katika maeneo ya elimu, sayansi, teknolojia, utawala, ardhi, mazingira, mazao ya kilimo, mifugo, sayansi ya jamii, uongozi, biashara, afya, mifugo, misitu na uvuvi kwa lengo la kuongeza maarifa na kutatua changamoto za jamii;
- itaandaa machapisho 379 ya tafiti katika maeneo ya elimu, ushirika, afya, usimamizi na uendelezaji ardhi, mazingira, makazi na ujenzi, uongozi; na
- itatoa mafunzo kwa watafiti kuhusu uandaaji na uchapaji wa majarida ya kisayansi ya ndani (Local Peer Review Scientific Journals) na viunzi vya uthibiti.
Serikali itaendelea kutoa tuzo kwa watafiti watakaochapisha tafiti katika majarida yenye hadhi ya juu kimataifa ili kuhamasisha watafiti wa ndani kufanya utafiti na kuchapisha kazi zao katika majarida husika.
Serikali itaanzisha programu itakayowawezesha vijana wanaohitimu katika ngazi mbalimbali za elimu kuendeleza mawazo ya ubunifu ili yawe biashara au kampuni changa (Talent Pool Program) kwa ajili ya kujiajiri au kuajiriwa. Aidha, itawawezesha vijana 20 wenye vipaji na wabunifu katika masuala ya uhandisi na teknolojia kupitia programu atamizi.
katika kuimarisha matumizi salama ya mionzi ya nyuklia nchini, Serikali kupitia Tume ya Nguvu za Atomu itatekeleza yafuatayo:
- itaendelea kudhibiti matumizi ya mionzi nchini kwa kukagua vituo 900 ikiwemo hospitali, vituo vya afya, migodi, viwanja vya ndege, na viwanda na majengo yenye mashine za kupima mionzi ili kuhakikisha uwepo wa mazingira salama kwa wagonjwa, wafanyakazi na umma kwa ujumla;
- itapima na kudhibiti viwango vya mionzi kwa wafanyakazi 2,110 wanaofanya kazi katika mazingira ya vyanzo vya mionzi katika hospitali, migodini na viwandani ili kuwalinda dhidi ya madhara yatokanayo na vyanzo vya mionzi sehemu za kazi; na
- itaendelea na upimaji wa sampuli 50,000 za vyakula, mbolea, tumbaku na bidhaa nyingine zinazoingia na kutoka nchini kupitia mipaka ya nchi ikiwemo viwanja vya ndege na bandari pamoja na sampuli za maji ya visima, wasambazaji na wamiliki wa viwanda ili kuwalinda wananchi dhidi ya madhara yatokanayo na mionzi.
katika kuimarisha utafiti wa tiba za saratani, Serikali itaanza utekelezaji wa Mradi wa Kituo cha Utafiti cha Tiba za Saratani (Oncology Research Centre) katika Jiji la Arusha ili kuleta tija na ufanisi katika kukabiliana na tatizo la saratani nchini pamoja na kuimarisha utafiti na uchunguzi kwa kutumia teknolojia ya nyuklia.
Serikali kupitia Tume ya Taifa ya UNESCO, itaendelea kuratibu, kuhamasisha na kusimamia utekelezaji wa mikataba na makubaliano ya kimataifa kwa kutekeleza yafuatayo:
- kuendelea kuiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika vikao na mikutano ya UNESCO kwa lengo la kutetea maslahi ya nchi;
- kuratibu na kufanya tathmini ya utekelezaji wa mikataba na makubaliano ya kimataifa ya UNESCO ambayo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeridhia kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utekelezaji; na
- kushirikiana na wadau katika kuhamasisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu.