Shirika la Masoko ya Kariakoo (KMC) linawataarifu wafanyabiashara na wananchi kuwa kutokana na maboresho yanayofanyika katika uendeshaji wa biashara katika soko jipya la Kariakoo na maagizo ya Serikali kutumia mifumo ya kielektoniki ili kuleta tija, Shirika litatumia mfumo wa kielektoniki wa TAUSI kutangaza maeneo ya biashara na kukusanya mapato.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam ,Kaimu Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko ya Kariakoo Bw. Sigsibert K.Valentine amesema, Shirika halitaruhusu mfanyabiashara mwenye deni la awali kupata umiliki wa eneo la kufanya biashara katika Soko la Kariakoo, hivyo amewataka wafanyabiashara wote wanaodaiwa kulipa madeni yao kabla ya kuomba tena nafasi ya kurejea kwenye maeneo yao ya biashara.
“Shirika la Masoko ya Kariakoo linadai jumla ya Shilingi 497,773,019.26 ambazo ni madeni yaliyolimbikizwa kwa muda mrefu. Madeni haya yanapaswa kuwa yamelipwa na wafanyabiashara kabla ya kurejea sokoni ili wapate nafasi ya kusajiliwa kwenye mfumo” alisisitiza Valentine.
Katika hatua nyingine ,Kaimu Meneja Mkuu huyo amemshurukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa shilingi Bilioni 28.03 zilizotumika kufanikisha mradi wa ujenzi na ukarabati wa soko la Kariakoo ambao kwa sasa umefikia asilimia 93.