Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa amesema hatasita kubadilisha timu ya Wataalam na Mkandarasi wanaoendelea na kazi ya kurejesha mawasiliano ya barabara ya Dar es Salaam- Lindi katika eneo la Nangurukuru kutokana na kasi ndogo ya kazi na usimamizi.
Bashungwa ameonesha hali hiyo ya kutoridhishwa na usimamizi na kasi ya urejeshaji wa mawasiliano katika eneo hilo na kumtaka Mtaalamu na Mkandarasi kuongeza kasi ili wamalize zoezi ndani ya muda uliotolewa.
“Mimi naweza kufukuza timu yote, bora niwaambie watanzania timu hii imefeli na niagize nyingine ambayo inaweza ikaja kufanya kazi, hatuwezi kwenda hivi”, amesema Bashungwa.
Aidha, Bashungwa amemuagiza Mkurugenzi wa Matengenezo ya Barabara – TANROADS kutafuta na kuongeza magari ya kubeba mawe na vifusi pamoja na mitambo ili kazi ifanyilke usiku na mchana bila kusimama.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Matengenezo kutoka Wakala ya Barabara (TANROADS), Dkt. Christina Kayoza ameahidi kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza katika eneo la Nangurukuru katika upande wa usimamizi na pia ameeleza kuwa amekwishafanya maandalizi ya upatikanaji wa mawe na mitambo ili yaweze kufika katika eneo hilo na kuongeza kasi ya urejeshaji wa miundombinu ya barabara yaliyokatika.