Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amezindua taarifa za utendaji katika Sekta ndogo ya Umeme, Gesi Asilia na Mafuta kwa mwaka 2022/2023 ambapo ametoa maelekezo mahsusi kwa Wizara na Taasisi mbalimbali kufanyia kazi taarifa hizo zinazoonesha mafanikio na changamoto katika Sekta Nishati.

Akizindua taarifa hizo tarehe 14 Juni, 2024 jijini Dodoma, Dkt. Biteko ameagiza Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati pamoja na Wizara ya Mipango na Uwekezaji kusoma taarifa hizo na kuzichambua na changamoto zilizoainishwa zipatiwe majawabu ndani ya kipindi cha miezi mitatu.

Aidha ameagiza kuwa, kila aina ya fursa iliyoonekana kwenye taarifa hizo ichukuliwe kwa uzito mkubwa na itambuliwe nani ana uwezo wa kuitumia fursa hiyo ndani ya Serikali na katika taasisi binafsi.

“ Vilevile nawaagiza EWURA mhakikishe kuwa, tathmini ya mwaka ujao ihusishe utendaji wa Nishati Safi ya kupikia ili kuweza kujipima kwa usahihi kuhusu utekelezaji wa ajenda hii inayopewa kipaumbele na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.” Amesema Dkt. Biteko

Agizo jingine ni kuwa, matishio yote ya Sekta ya Nishati yaliyoainishwa katika ripoti kati ya mwaka 2023 hadi 2025 yawekewe mabunio ya suluhisho lake ili katika ripoti ijayo changamoto husika zisiwepo ikiwemo suala la kuongezeka kwa mahitaji ya umeme kila mwaka.

Dkt. Biteko pia ameitaka EWURA kupima uhusiano wa rasilimali zilizopo na mafanikio ya watu ambapo amesisitiza kuwa mafanikio ya sekta lazima yaendane na mabadiliko ya maisha ya watu.

Pia ametaka mifumo ya uagizaji mafuta iendelee kuboreshwa baada ya kufanyika utafiti wa kina na kueleza kwamba miundombinu ya mafuta bado inahitajika huku akisisitiza kuwa urasimu usiwepo kwenye Sekta ya Nishati.

Ameipongeza  EWURA kwa tathmini ambayo inaonesha kuwa Sekta ya Nishati inaendelea kuimarika, akitolea mfano kutolewa kwa leseni ya kuchimba gesi asilia katika kisima cha Ntorya kilichopo mkoani Mtwara kitakachotoa gesi futi za ujazo milioni 140 kwa siku ambapo leseni ya mwisho ya kuchimba gesi ilitolewa mwaka 2006.

Kuhusu sekta ndogo ya umeme amesema amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuiboresha ambapo leo ametoa taarifa kuwa mradi wa Julius Nyerere (JNHPP) umeingiza mtambo wa pili katika gridi ya Taifa kupitia mtambo namba 8 na hivyo kufanya mradi huo kuingiza megawati 470 katika gridi.

Kuhusu sekta binafsi amesema, “Sekta binafsi imetutoa kimasomaso, Serikali haiwezi kufanya kila kitu, wamefanya kazi kubwa mno kwenye mafuta, gesi na hata kwenye uzalishaji umeme, wito wangu kwenu msibaki nyuma changamkieni fursa, na kwa taasisi zilizo chini ya Wizara msione sekta binafsi kama watu wajanjawajanja, tuwape kipaumbele.” Amesema Dkt. Biteko

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiimarisha Sekta ya Nishati na kusema kuwa Dodoma imeshuhudia matunda ya uimarishaji huo wa sekta kwani sasa umeme haukatiki.

Pia amepongeza utashi mkubwa wa uongozi wa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ambao unachangia kwa kiasi kikubwa katika kuiimarisha Sekta kwa ujumla.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema kuwa katika tathimini iliyozinfuliwa inaonesha sekta imepiga hatua kwenye maeneo megi ikiwemo uhakika wa upatikanaji umeme, upatikanaji na usambazaji wa mafuta kuimarika hasa baada ya Dkt. Doto Biteko kuanza kuongoza Wizara ya Nishati, aidha upatikanaji na uwekezaji wa gesi unaendelea kuimarika na hii ikijumuisha usambazaji gesi kwenye maeneo mbalimbal .kama magari, majumbani na viwandani.

Ameongeza kuwa, taarifa ya Benki ya Dunia kwa nchi za Dunia ya Tatu zinazofadhiliwa na Benki hiyo inaonesha kuwa Sekta ya Nishati kwa Tanzania inafanya vizuri zaidi katika nchi zote zinazoendelea na Bara la Afrika kwa ujumla na hii matunda ya usimamizi madhubuti wa Dkt. Doto Biteko ambapo  eneo lililofanya vizuri zaidi ni usambazaji umeme vijijini na miradi mingine ya nishati kama JNHPP na mradi wa TAZA.

Ameongeza kuwa Benki ya Dunia imeidhinisha Dola.za Marekani milioni  300 ili ziendeleze sekta ya umeme kutokana na ufanisi huo wa Tanzania.

Akitoa taarifa za utendaji katika Sekta ya Nishati, Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Andilile alisema kuwa Sekta ya Nishati inaendelea kuimarika ikiwemo uwekezaji kwenye miundombinu ya mafuta, uwekezaji wa vituo vya mafuta na maghala umeongezeka, kuna ongezeko la uagizaji wa Gesi ya Mitungi (LPG) kwa asilimia 16 na ongezeko la uagizaji wa mafuta kwa asilimia 8.

 Amesema kuwa katika Sekta ya umeme uwekezaji umeongezeka katika uzalishaji, usafirishaji na usambazaji, upotevu wa umeme unazidi kupungua na wateja wa umeme wameongezeka kutoka milioni 3.8 mwaka 2021/22 hadi milioni 4.4 mwaka 2022/2023.

Baadhi ya  changamoto zilizoainishwa kwenye taarifa katika sekta ya umeme ni uchakavu wa miundombinu ambao unaendelea kufanyiwa kazi na uwekezaji endelevu kwenye sekta.