Hatua hii itachochea kasi ya kupungua kwa vifo vya akina mama wanaojifungua pamoja na watoto wachanga kutokana matatizo yanayohusiana na upungufu wa damu mwilini, na kupungua kwa kinga mwili. Vilevile, itapunguza matatizo ya vichwa vikubwa na mgongo wazi kwa watoto
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka Mikoa yenye viwango vikubwa vya upungufu wa damu na udumavu ianze kutekeleza mpango wa urutubishaji wa chakula kuanzia ngazi ya vijiji ili baada ya miaka mitano kuanzia sasa zaidi ya nusu ya Watanzania wawe wanatumia chakula kilichorutubishwa.
“Hatua hii itachochea kasi ya kupungua kwa vifo vya akina mama wanaojifungua pamoja na watoto wachanga kutokana matatizo yanayohusiana na upungufu wa damu mwilini, na kupungua kwa kinga mwili. Vilevile, itapunguza matatizo ya vichwa vikubwa na mgongo wazi kwa watoto.”
Pia, Waziri Mkuu ameitaka Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais TAMISEMI pamoja na wadau wote wa lishe washirikiane katika kuandaa mkakati mahsusi wa kuelimisha umma na kuhakikisha wananchi wanapata uelewa mpana wa umuhimu wa virutubishi vinavyochanganywa kwenye chakula katika kukabiliana na changamoto za lishe duni.
Ametoa maagizo hayo leo (Jumamosi, Juni 15, 2024) wakati wa Uzinduzi wa Kiwanda cha Kutengeneza Virutubishi na Tovuti ya Wasindikaji Chakula Tanzania kilichipo Mikocheni jijini Dar es Salaam. Amesema ili kulinda afya za walaji, wasindikaji wote wazingatie namna ya kutunza virutubishi na vinyunyizi vya virutubishi ili visiharibike. Kiwanda hicho ni cha kwanza kwa Afrika Mashariki na cha pili kwa Afrika.
Waziri Mkuu amesema uzinduzi wa kiwanda hicho ni sehemu ya mkakati mpya wa juhudi za Serikali na washirika wake katika kuwezesha usindikaji bora zaidi na uwekaji virutubishi kukidhi mahitaji ya mwili. “Urutubishaji huo utaendelea kupunguza viwango vya vifo vya akina mama wanaojifungua pamoja na vifo vya watoto wachanga vinavyotokana na matatizo yanayohusiana na upungufu wa damu mwilini.”
Amesema urutubushaji huoutaimarisha afya ya watoto wa kike walio katika rika balehe kwa kuwapunguzia changamoto ya upungufu wa damu, vilevile utasaidia kuimarisha afya za watoto kwa kukabiliana na tatizo la kupungua kinga mwilini ambalo ni chanzo cha watoto kuugua mara kwa mara, lakini pia kupunguza matatizo ya vichwa vikubwa, mdomo sungura na mgongo wazi kwa watoto.
Akizungumzia kuhusu uzinduzi wa tovuti ambayo ni mahsusi kwa ajili ya mtandao wa wasindikaji wote wa chakula hasa unga na mafuta ya kula, Waziri Mkuu amesema mtandao huo una manufaa makubwa kwani pamoja na mambo mengine, unakusudiwa kutumika katika kutoa elimu na kuongeza ujuzi kutoka kwa wasindikaji wakubwa waliobobea kwenye teknolojia ya usindikaji chakula hapa nchini na kwingineko duniani.
“Vilevile, ni fursa nyingine nzuri kwa wasindikaji kujiendeleza kwani nimearifiwa kuwa kupitia tovuti hiyo, wasindikaji wataunganishwa na wafadhili na kupata misaada mbalimbali. Misaada hiyo itawawezesha kuboresha mifumo ya usindikaji pamoja na uhakiki wa ubora na viwango vya virutubishi katika chakula.”
Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema mpaka sasa, Mikoa yote 26 ya Tanzania Bara ina wazalishaji na wafungashaji wa unga wa mahindi 1,282 wanaoongeza virutubishi katika bidhaaa hiyo.
Amesema hatua hiyo imefikiwa kwa ushrikiano na wadau wa lishe hasa wanaosaidia afua hii ya urutubishaji wa vyakula, ambapo katika bajeti ya 2023/24 Wizara ya Afya ilitenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa vinyunyizi 300 (dosifiers) vya virutubishi wakati wa kusaga nafaka hususan unga wa mahindi na ngano na kufungwa katika vinu 300 katika halmashauri mbalimbali Nchini.
“Kwa mwaka huu mpya wa fedha 2024/25 tumetenga kiasi cha bilioni moja katika bajeti yetu kuendelea kununua tena vinyunyizi ili urutubishaji uifikie jamii kubwa zaidi na kupunguza matatizo ya lishe niliyoyataja hapo juu.”
Naye, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe amesema suala la kuimarisha lishe kupitia uongezaji virutubishi viwandani limekuwa likifanyika kwa viwanda vikubwa tu tangu mwaka 2013 hasa kwa viwanda vya kuzalisha unga wa ngano na mafuta ya kula.
Ameongeza kuwa kwa sasa Serikali imeendelea na jitihada za kuhakiksha wazalishaji wadogo nao wanaongeza virutubishi kwani kwa asilimia zaidi ya 80 ndio wanaolisha watu wengi zaidi.
Amesema wazalishaji wadogo hasa wasindikaji wa unga wa mahindi na mafuta ya kula walikuwa wanakabiliwa na changamoto ya teknolojia ya kuongeza virutubishi ambayo kwa sasa tumejihakikishia kuwa teknolojia hizo zipo za kutosha. Serikali
Awali, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga amemuhakikishia Waziri Mkuu kwamba wataendelea kushirikiana na wadau katika kuratibu mpango wa lishe ili kuhakikisha linaendelea kupewa kipaumbele.